Kesi ya Capital FM na Nation, yaashiria Utumwa ndani ya Media?Nation na Standard leo Marafiki?

Kwamba waandishi wa habari ni mali ya mashirika wanayoyafanyia kazi na hawana uhuru wa kutoa mawazo yao kinyume na sera za mashirika yao, hiyo nilikuwa ninajua. Lakini sikujua kwamba hawaruhusiwi kujiunga na shirika jingine wakati wowote wanapojisikia kufanya hivyo, mpaka niliposoma kwenye magazeti kwamba Capital FM wamewashitaki Nation FM kwa kile walichokiita kuwanyanganya mali yao bila kuwapa taarifa.

Siyo kwamba naandika haya kuwatetea Nation FM, maana hata wao hawakufanya vizuri kuanzisha radio mpya na kuwaajiri watangazaji ambao tayari tulikwisha wasikia kwenye vituo vingine vya FM. Maana ni sawa na kutengeneza soda mpya yenye ladha ya Coca cola ukifikiri unawamaliza, kumbe kwa njia moja au ile nyingine unawainua waanzilishi wa ladha hiyo bila wewe kujua.

Lakini mimi nautetea uhuru wa waandishi wa habari kuajiriwa popote wanakotaka, na kutoa mawazo yao hata kama ni kinyume cha sera za mashirika wanayoyafanyia kazi maana ni sera hizo ndizo zinazochangia kuwepo kwa wahariri watakaohakikisha kuwa mawazo ya waandishi yanaenda sambamba na kile wanachokiita sera za mashirika hayo, lakini mimi nauita huo utumwa wa kimawazo.

Sina utaalamu wa kisheria kuamua kesi hiyo,lakini uhuru wa mtu yeyote kufanya kazi popote unapoingiliwa na mikataba yenye lengo la kuwatumia wafanyakazi kama watumwa, wasioweza kulihama shirika kwa sababu tu waliingia ubia wa kimaandishi, inanipa wasiwasi mkubwa na kunifanya niifuatilie kesi hiyo kwa karibu sana kuuona mwisho wake.

Lakini mambo yakiwa hivi, ni vizuri kuangalia kwa makini mikataba yote kabla ya kuweka saini.

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili2 | Nyimbo Za Munishi | Next >>