Tamasha la nyimbo za Injili, Kutangaza KTN na STANDARD Haitoshi mngefanya zaidi |
Kwamba mashabiki wengi wa nyimbo za injili wangependa kununua kaseti wakasikilizie nyumbani kuliko kuwasikiliza wasanii wenyewe wakiimba, hizo ni habari njema kwa wasanii wa Injili ukiwalinganisha na wenzao wa upande wa pili ambao mashabiki wao wanapenda kuwaona wakiimba lakini hawanunui kaseti zao. Kwa wasanii wa injili habari hizo ni njema kipesa, lakini ni mbaya kisanaa.Na hii inaungwa mkono na ukweli kwamba ni wasanii wachache sana wa Injili wanaoweza kuwatumbuiza mashabiki wao hadharani mpaka mashabiki waridhike . Kwa hiyo wazo la kufanya tamasha la nyimbo za Injili Nyayo stadium bila malipo haliwahakikishii watayarishaji kuwa watu watakuwa wengi kwa sababu tu hawalipi. Kulipa au kutokulipa hakuleti tofauti kubwa sana,ila wanalipa ili kuona nini hiyo ndiyo ya muhimu kwa mashabiki. Ni mashabiki wachache sana watakaokubali kulipa pesa ili wakawaone watu wanaofanya kitu ambacho hata wao wanaweza kukifanya vizuri kuliko hao wanaojiita wasanii. Yaani kuweka kaseti na kuifuatilizia inavyoimba. Waimbaji karibu wote wa nyimbo za Injili wanatumia mtindo rahisi wa kuimba huku wakifuatilizia kaseti,mtindo ambao ulioteshwa mizizi na KBC TV ambao ndio waliojenga mwamko wa nyimbo za Injili siyo tu katika Kenya, ila Afrika ya mashariki na kati kwa ujumla. Kuanzia mwaka 1984 shirika la utangazaji la kenya KBC likitumia vipindi ‘Sing and Shine’,pamoja na ‘Joy Bringer’shukrani zimwendee Karanja Kimwere, lilianza kuwainua wasanii wa nyimbo za Injili mpaka ikafikia kiwango cha kuhatarisha maisha ya zile nyimbo nyingine za dansi ambazo mpaka leo hazijazinduka kutokana na kipigo hicho. Lakini KTN walipoanza kurusha matangazo yao, hawakuona umuhimu wowote wa kuwasaidia wasanii wa injili wakati huo badala yake walilinua shirika la kimarekani CNN ambao mpaka leo KTN hawawezi kushindana nao kitaaluma, au kipesa. Ilikuwa kama kumfuga mnyama ambaye atakua mpaka abomoe nyumba yako na kuanza kula watoto wako.Hayo ndiyo KTN waliyoyafanya wakati huo. Lakini wahenga ‘walisema yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yanayokuja.’ Sasa KTN wakishirikiana na gazeti la STANDARD wanakuletea kile wanachokiita ‘uimbaji wa kufunga Karne’. Bila kuwavunja moyo naipongeza hatua waliyoichukua ya kuwakumbuka wasanii wa Injili mwishoni mwa Karne, bila kusahau kuwakumbusha kuwa wakiona vinaelea wajue viliundwa. Lakini ingekuwa busara zaidi kama wangeanza mapema kama miezi sita nyuma kuunda hiki wanachotaka kitokee jumamosi Nyayo Stadium.Kama KBC walivyotumia miaka 15 kutengeneza kile wanachokiona sasa kama nyimbo za Injili, na wao angalau wangetumia miezi sita ya kurekodi na kuzirusha hewani nyimbo za injili ambazo zimeimbwa na kuchezwa vyombo kwa wakati mmoja hadharani, ili kuondoa ule ukiritimba ulioko sasa wa waimbaji kuimba huku wakifuatia kanda , jambo ambalo linawafanya mashabiki wawe na wasiwasi kuwa hizo nyimbo ni za wasanii wahusika? au ni za wasanii wengine na hawa wanaigiza tu. Hasa ukitilia maanani kwamba siku hizi ukiwa na pesa unaweza kuwalipa wachezaji wa kulipwa wakapanga na kucheza kaseti nzima na kesho ukaitwa mwimbaji wa nyimbo za Injili na kumbe hujui hata noti moja ya nyimbo unazoimba. Lakini Jumamosi ndiyo siku ya siku.Maana waliozoea vya kunyonga, vya kuchinja hawaviwezi Imeandikwa na Faustin S. Munishi. |