Maajabu ya Karne wakati Maadui wa jadi!
|
Maneno ya Mwokozi wetu Yesu Kristo kwamba “Mpende adui yako” yameanza kutimia wakati magazeti ya ‘Nation’na ‘Standard’yalipotangaza kwa pamoja kuwaomba watu wanaojisikia kufanya kazi ya kuuza magazeti yao mjini Nairobi wajitokeze kwa wingi kuifanya kazi hiyo ambayo malipo yake hayatoshi kutoka mkononi kwenda mdomoni. Mwito huo ulifuatia baada ya wale waliokuwa wakiifanya kazi hiyo hapo awali kugoma kuyauza magazeti hayo,wakidai katiba za magazeti hayo zibadilishwe ili kipengele kinachomruhusu mhariri kulipwa pesa nyingi kuliko wale wengine na wauzaji wakiwemo, kibadilishwe.Pia walidai kuwa, kwa sababu magazeti hayo yamekuwepo kwa muda mrefu yamekosa mwelekeo kwa hiyo yaachie ngazi ili magazeti mapya kama ‘People’na ‘Kenya Times’pamoja na magazeti kama yale ya ‘Injili’ na ‘Matatu Times’yatoe hoja mpya. Ama kwa kweli hii ni karne ya kubadilisha katiba na kungatuka.Lakini badala ya magazeti hayo kusikia kilio cha wauzaji hao, wao wamesema hawatangatuka ng’o! Na wala hawatabadilisha katiba yao iwe katiba inayoendeshwa na wauzaji,badala yake itabaki kuwa katiba inayoendeshwa na wawekezaji wa raslimali kwenye magazeti hayo, pamoja na wahariri.{Gazeti la Nation mwekezaji wa raslimali ni Agha Kan, na wakati lile la Standard ni kampuni moja ya Uingereza, na yamekuwepo hata kabla ya hao wauzaji kuzaliwa.} Kipengele kingine wanachodai kibadilishwe ni kile kinachomruhusu mhariri kuhariri habari za waandishi wengine jambo ambalo linawafanya wauze habari ambazo ni mawazo ya wahariri pekee kinyume na inavyotakiwa kuwa. Jambo hilo wamedai linampa mhariri nguvu nyingi kiasi cha kuweza kumtuma ripota kwa mwanasiasa,au mtu yeyote anayetaka kummaliza na kuagiza akaulizwe maswali aina fulani ya kupiga mhuri stori ambayo tayari mhariri amekwishaitayarisha na kuipa mwelekeo. Kama mgomo wa hao wauzaji utaleta mabadiliko katika vyombo vya habari tunasubiri tuone. Lakini ujumbe ambao hawawezi kuupuuza ni kwamba wakati wa kuwa peke yao uwanjani umekwisha na sasa kuna wapinzani wengi tena wenye mbinu mpya.Kama wanavyosema kiongozi akikaa sana madarakani hulewa madaraka, pia gazeti likikaa sana na lenyewe huanza kulewa madaraka na kuanza kwenda kinyume na taaluma ya uandishi. Lakini urafiki wa hawa wazee wawili waliokuwa maadui zamani una lengo la kuwafanya wadumu katika biashara hata kama haijulikani kama bado ‘Nation’ ndio wanaoongoza katika mauzo ya magazeti kama walivyozoea kudai, maana kila gazeti jipya linapoanzishwa, linakata sehemu ya wasomaji kutoka kwa wakongwe hawa wawili. Bila kuwasahau ‘Kenya Times’ambao wanajulikana kama watoto wa KANU, nao pia wanawatoa jasho hawa mababu wa kale.Ukija upande wa ‘THE PEOPLE’ wanaojulikana kama watoto wa upinzani wanawahemesha hawa vikongwe sawa sawa hasa baada ya kuanza kutoka kila siku.Tena wameacha ule wimbo wa ‘Moi must Go’maana wamegundua hata kama akienda watabaki wakiandika nini? kwa hiyo siku hizi wanaimba kila wimbo jambo ambalo limewapa mashabiki hata kutoka KANU,na hizo zote ni habari mbaya kwa hawa wanaojiita majabali wa habari. Lakini kipesa ‘Nation’ wanaonekana wako mbele ya ‘Standard’ maana wana jengo lao wenyewe japo lina sura mbaya kuliko majengo yote Nairobi.na pia wana mitambo yao wenyewe ya kuchapishia magazeti jambo ambalo linawaweka mbele ya wapinzani wao wa jadi. Tunapoigia kwenye karne mpya ya sayansi na teknolojia lazima kila kitu kibadilike ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari.Watakaokataa kubadilika watapitwa na wakati maana hata wale wanaotangaza matangazo hawajui watangaze kwenye chombo kipi cha habari ili tangazo lao lionekanae na wingi wa watu, maana wote wanategemea matangazo ya biashara kuweza kudumu katika biashara yao ya kusema chochote mradi kiwavutie wasomaji au wasikilizaji. Lakini inapokuwa kwamba ni lazima mfanyibiashara atangaze kwenye vyombo vyote vya habari ndipo aweze kuwafikia watu wengi na ujumbe wake, kama bei za kutangaza siyo za chini sana, itambidi aache kutangaza kabisa. Na matokeo yake ni kwamba waandishi watakosa pesa na wakimuona yeyote anayepata pesa kwa halali watamshambulia. Imeandikwa na Faustin S.Munishi. |