Moja ya haki za
wanaume katika jamii ni kuiongoza jamii, na siyo Kuwaachia Wanawake kazi
hiyo. Kuwapenda wake zao na siyo kuwapiga. Kutumia nguvu walizopewa kuilinda
jamii na siyo kuinyanyasa. Kufanya kazi kwa bidii kuilisha jamii na siyo
kuzurura ovyo bila kazi. Wanaume walionyan’ganywa haki hizo wanatakiwa
waanze kuzitetea haki zao sasa na siyo baadaye. Hapo mwanzo Mungu alimuumba
Mtu wa kwanza. Mwanamume kutoka katika mavumbi na kumpulizia pumzi yake
akawa kiumbe hai. Na baadaye aliona si vema huyo Mwanaume akae peke yake,
alitwaa ubavu wake akamtengenezea msaidizi yaani Mwanamke. Aliwaweka katika
bustani ya Eden ambapo aliwaruhusu kula matunda yote isipokuwa tunda la
mti wa katikati. Shetani akitumia umbo la nyoka, alimdanganya mwanamke
akala tunda ambalo Mungu alikataza. Siyo kwamba alikula yeye tu, bali
alimdanganya na Mwanaume akala pia. Shetani akamdanganya Mwanamke, na
mwanamke akamdanganya Mwanaume, dhambi ikaingia ulimwenguni. Ni baada
ya dhambi kuingia, ndipo kila mmoja Mwanaume na Mwanamke akapata laana
zake ambazo ziliambatana na majukumu ya kila mmoja katika jamii. Ni wakati
huo ndipo Mungu aliposema: “Kwa sababu umefanya hayo ewe nyoka, umelaaniwa
wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni, kwa
tumbo utakwenda na mavumbi utakula siku zote za maisha yako. Nami nitaweka
uadui kati yako na huyo Mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake, huo
utakuponda kichwa nawe utamponda kisigino.” Akamwambia Mwanamke: “Hakika
nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako, kwa utungu utazaa watoto,
na tamaa yako itakuwa kwa mumeo,naye atakutawala.” Akamwambia Mwanamume:
“Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza
nikisema, usiyale, ardhi imelaaniwa kwa ajili yako, kwa uchungu utakula
mazao yake siku zote za maisha yako, michongoma na miiba itakuzalia, nawe
utakula mboga za kondeni, kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata
utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa, kwa maana u mavumbi
wewe nawe mavumbini utarudi.” Mwanzo: 3: 14-19. Tangu wakati huo, majukumu
ya Mwanaume katika jamii yamekuwa kuingoza jamii huku akifanya kazi ngumu
kwa jasho kama alivyoagizwa na Mungu mwenyewe. Tatizo kubwa tulilo nalo
siku za leo, ni Wanaume walioyaacha majukumu yao ya kuiongoza jamii, na
kuipelekea jamii kubaki bila kiongozi. Wanaume wanaposhindwa kuchukua
nafasi zao za uongozi katika jamii, basi matatizo mengi hutokea. Bila
shaka matatizo tuliyo nayo leo, mengi kama si yote yamesababishwa na uongozi
hafifu katika nyanja zote za maisha. Mwanaume anaposhindwa kukaa na jamii
yake nyumbani, na badala yake kupoteza muda mwingi nje ya nyumba yake,
matokeo ni nyumba yake inakosa uongozi, na watoto wanaanza kuwa na tabia
ambazo hata waalimu hawawezi kuzirekebisha kwani hata waalimu baadhi yao
siyo viongozi wazuri wa jamii. Wazazi tena wote wawili wana jukumu kubwa
la kuwalea watoto lakini zaidi mzazi kiongozi ambaye ni Mwanaume. Jukumu
hilo linapoachiwa waalimu au viongozi wa Dini matokeo yake mara nyingi
hayawi mazuri kwani hata viongozi wa Dini siyo wote wazuri. Na kama kazi
ya kulea ni ngumu, basi kwa nini mlizaa? hili ni swali langu kwa wale
wazazi wanaowaona watoto kama kero. nasema ni kero kwa sababu utawakuta
wazazi Mungu amewabariki wana kila kitu wanachokiitaji kuwalea watoto,lakini
hawafanyi hivyo. Badala yake wanawapeleka watoto shule za kulala wakiwa
bado wadogo, sababu ni eti wanawapenda ndio maana wanafanya hivyo. Lakini
uchunguzi uliofanywa na Injili unaonyesha kuwa, siyo upendo unaowafanya
wazazi kuwahamisha watoto nyumbani, wakati wanahitaji kujifunza mengi
kutoka kwa watu waliowaleta duniani, bali wazazi wengi wanataka ule usumbufu
wa watoto uwaondokee, wakae kwa utulivu nyumbani bila kelele za watoto.
Na chuki ya watoto siyo kwamba inaanza tu wanapokuwa na umri wa kwenda
shule, kwa wazazi wengine chuki hiyo inaanza pale mtoto anapozaliwa, maana
tangu akiwa mdogo amekuwa akilelewa na mfanyakazi kwa muda mrefu kuliko
na wazazi wake. Utasema alikuwa mdogo hakumbuki. Usidanganyike! anakumbuka
yote ndio maana hana uhusiano wa karibu na wazazi. Kwa sababu anajua muda
aliokaa na wazazi hautoshi kujenga uhusiano wa karibu na wao badala yake
anawaona kama wageni wanaokuja nyumbani kwao usiku na kuondoka asubuhi.
Pamoja na uhusiano mdogo ulioko kati yao, bado wazazi wanaamua kumtupia
huyo mtoto waalimu ambao na wenyewe ya kwao yamewashinda, na sijui wanamini
vipi kwamba watayaweza ya wenzao. Ukweli ni kwamba hawayawezi. ndiyo maana
watoto wanaanza tabia mbaya shuleni na wazazi wakitaka kuingilia kati
kuwarekebisha wanakuwa wamechelewa, maana samaki usipomkunja akiwa mbichi,
akiishakauka hakunjiki tena. Kwanza wanawaona wazazi ni wageni ambao muda
mwingi wa maisha yao hawajakaa na wao, Pili wanawaona ni kama watu wa
karne ya saba waliopitwa na wakati. Tatu kwa sababu hawakuwahi kupokea
amri kutoka kwa wazazi walipokuwa wadogo, hawatakuwa tayari kuzipokea
ukubwani. Na wale ambao wazazi walidhani kuwa watawapa amri kwa niaba
yao, kumbe amri zao zote hazikuwa zinafuatwa kwani hakuna mtu mkubwa kwa
mtoto kama mzazi. Nne tunakuwa na vijana ambao hawapokei amri kutoka kwa
yeyote. Na wakati wa likizo wazazi wanajaribu kuwaomba wakae na wao nyumbani,
na wao wanasema hawawezi kukaa na wageni wa karne za nyuma, wanatoka kwenda
kukaa na watu wa karne ya ishirini na tano, ambayo ni karne ya kuona video
zenye picha chafu, pamoja na kusikia miziki ya “Ndom-” Nisimalizie maana
na mimi nitakuwa nimesema matusi. Siyo hivyo tu; bali hata nguo zao ni
zile zinazopwayapwaya, pamoja na madawa ya kulevya. Na mchezo wa matusi
ndiyo chakula chao. Niseme nini? Kusaidika labda Mungu mwenyewe awasaidie,
maana hata Makanisa yaliyoko sasa wakienda wanaambiwa watoe ndiyo wabarikiwe
na wao hawana cha kutoa labda watoe “bangi’. Lakini Yesu ni yeye jana
leo na hata milele. vijana wakitubu watasamehewa. Ndiyo maana ni vigumu
kuongea kuhusu haki za Wanaume au Wanawake bila kutaja watoto. Pamoja
na kwamba Wanawake wamekuwa na vikao vingi vinavyodai haki zao, kwangu
mimi naona wanaume ndiyo wangetakiwa wawe na mikutano mingi ya kudai haki
zao lakini cha ajabu ni kwamba hawajafanya hata mmoja. Swali ni kwa nini?
ni kwa sababu hawajanyimwa haki zao? au wanajikaza kisabuni? Jibu wanalo
wenyewe. Kwa vyovyote vile, wanaume nao wana matatizo yao ambayo wakipata
nafasi ya kusema yale ambayo wanawake wanawatendea, utawahurumia. Sasa
basi ikiwa Wanawake watakuwa na mkutano wao Beijing wa kuwalaumu Wanaume
bila wao kujitetea, na Wanaume nao wawe na mkutano wao Nairobi unaowalaumu
Wanawake kwa mabaya wanayowafanyia Wanaume ambayo ndiyo mengi, nani atakuwa
mwamuzi? Inavyonekana Mtoto ndiyo anayetakiwa aamue ugomvi huo wakati
naye ana matatizo yake yaliyosababishwa na Wanawake na Wanaume. je ataamua?
Au ataeleza matatizo yake? Nionavyo mimi Wanawake walikosea kwenda Beijing
peke yao na kuwalaumu Wanaume mbele ya watoto. Wangetakiwa kama watu wazima
wawaite Wanaume waende wote Beijing, waongee na wamalize tofauti zao.
Lakini sasa wameshaharibu maana wameshasema yote, inabidi Wanaume nao
waseme yote; ili waamuzi waamue baada ya kusikia kutoka pande zote mbili.
Kauli ya wanaume Nani amenyimwa haki? Kama si Mwanaume wakati anapodanganywa
na Mwanamke amwache Mwanamke aende kwa Mwanamke? Usidanganyike; Wanaume
ndiyo wamenyimwa haki zao tangu mwanzo. Na Wanapojaribu kuzidai hata wengine
wamepoteza maisha yao. Nayakumbuka maneno niliyoambiwa na babu yangu,
nikiwa kijana wa miaka kumi na nane nilipoingizwa Jandoni kwamba; “Mjukuu
wangu utakapofikisha umri wa kuoa; jiadhari sana na Mwanamke, kwani anaweza
kukuua wakati wowote; Boma ni lako lakini usiingie kimya kimya; kwa nini
ufe kabla ya wakati wako? Kohoa kwanza au fanya ishara yeyote kuwaashiria
walio ndani kuwa mwenye boma anakuja. Mpe adui nafasi ya kutoroka maana
mkikutana kifuani mmoja kati yenu atakufa; Na kwa nini ufe kwa ajili ya
asali ambayo huwezi kuimaliza?” Sikuyatilia maanani maneno hayo, lakini
miaka ilivyoendelea niliona Wanaume ndiyo wanaokufa kwa wingi kuliko wanawake;
Na hata sasa ninapoandika Wanawake waliofiwa na Waume ni wengi kuliko
Wanaume waliofiwa na Wake. Kwamba Wanaume wanakufa vifo vya kawaida, au
wanawake wana mchango katika vifo vyao, hiyo sijui; Lakini maneno ya Babu
sasa nayatilia maanani. Niseme nini juu ya Mwanaume aliyekuwa na mali
nyingi na sasa mali zote zimeisha baada ya kudangaywa na Wanawake? Nani
amenyimwa haki hapo Mwanaume au Mwanamke? Unakumbuka kisa cha Samsoni
na Delila? Wakati delila alipomdanganya Samsoni akasema siri zote mpaka
ikasababisha Samsoni kun’golewa macho na Wafilisti; Nani aliyenyimwa haki
hapo? Mwanamke au Mwanaume? Muone huyu mwanamke anayewaaribu vijana wadogo
wa kiume, akitumia pesa alizomwibia Mumewe, anawafanya watumwa wa kimapenzi
pamoja na kuwanyanyasa kijinsia, nani anayenyimwa haki hapa; Mwanume au
Mwanamke? Nasema wakati wa kuamka kwenye usingizi umefika; Tumenyanyaswa
na Wanawake vya kutosha. Na sasa tunataka mageuzi ya kutufanya tisinyanyaswe
tena. Walienda Beijing tukanyamaza, Wakafikiri sisi ni wajinga; Sasa tumejua
lengo lao, na hawatafanikiwa. Haki ya kuongoza jamii ni ya Mwanaume, na
kamwe hatutawaachia wanawake kazi hiyo. kufanya hivyo tutamkosea Muumba
aliyetupa jukumu hilo. Huo ndio msimamo wa Wanaume. Pamoja na kuusikia
msimamo wa Wanaume Injili nayo inasema, Matatizo ya Wanawake yamesababishwa
na Wanawake wenyewe na yatatatuliwa na wao wenyewe. Kwa hiyo siku nyingine
wakiwa na mkutano kama ule wa Beijing, wawaambie wenzao wa kike waache
kuwaharibu Waume zao. Vivyo hivyo yale ya Wanaume nayo yatatatuliwa na
wao wenyewe. La muhimu ni kwamba, baada ya kelele zote Wanawake watabaki
kuwa Wanawake tu. Na Wanaume nao watabaki kuwa viongozi wa jamii tu. Lakini
matatizo ya Watoto hayawezi kutatuliwa na wao wenyewe, kwa sababu hawakuyasababisha
bali yalisababishwa na Wazazi wa kike na wa kiume. Haya yatatatuliwa na
wanawake pamoja na Wanaume bila kuwaacha Watoto. Kwa hiyo mkutano ujao
uwe wa Watoto na wazazi wa pande zote mbili. Huu ndio mkutano wa jamii.
Na mwandishi wa Injili Munishi. |