Nyerere alishindwa mambo mengi
|
Kiafrika Mtu akishakufa siyo vizuri kuusema ubaya wake maana mwenyewe hayuko kujitetea. Lakini anapokuwa hai, hata kama ni uhai unaosaidiwa na mitambo, bado watesi wanaruhusiwa kuusema ubaya wake ili akipona ajirekebishe.Na asipopona basi itawabidi watesi wanyamaze kimya wawasikilize mashabiki wake wakisema uzuri wa Mwalimu wa kuwakomboa Watanzania kutoka katika minyororo ya ukoloni wa Waingereza na kuwaigiza kwenye ukoloni mwingine wa Julius Kambarage Nyerere. Ukoloni wa kwanza haukuwa mbaya kuliko huu wa pili,ila tofauti yake ni kwamba ukoloni wa pili uliongozwa na Mwafrika kutoka Butiama, na ule wa kwanza uliongozwa na mzungu kutoka Uingereza. Kwa hiyo tofauti ilikuwa ni viongozi wa ukoloni, na Watanzania hawakutoka katika minyororo ya ukoloni, bali walibadilika kutoka ukoloni huu kungia mwingine ambao ndio unaowatawala mpaka leo. Kwa watu wenye mawazo kama mimi, ni heri tungebaki kama tulivyokuwa maana msaada wa kweli ungetoka popote, kuliko kujidanganya kuwa tulikuwa salama na kumbe ukweli wa mambo ni kwamba tulikuwa pabaya kuliko mwanzo.Ilikuwa kama kukimbia mvua na kuingia kwenye kibanda cha nyasi kinachovuja. huwezi kueleza tofauti maana bado unanyeshewa. Na mpaka leo Watanzani kama mimi hatujui tofauti ya kuwa huru na kutawaliwa.Ikiwa kuwa huru ni kumruhusu Nyerere kujaribia mawazo yake ya siasa ya ujamaa kwenye maisha yetu na baada a miaka 30 atuambie mawazo yake yalishindwa kwa sababu alikosea, na adhabu tuliyompa ni cheo cha baba wa Taifa, basi mtanisamehe nikisema kuwa mwacheni huyo mzee apumzike kwa amani kutoka katika dunia hii, ili akapate nafasi ya kukutana na Muumba wake ambaye akiamua kumsamehe amsamehe. Na pia akiamua kumhukumu yote ni sawa, lakini siwezi kumwomba Mungu amponye Nyerere aje kufanya nini? Ambacho hakukifanya kwa miaka yote 77 aliyoishi duniani? alitumia nusu ya maisha yake kufanya majaribio na Watanzania,na sasa Mungu atatushangaa kwamba tunamsumbua amponye. Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu, na hawezi kukubali kushiriki utukufu wake na Nyerere.Amewaona Watanzania wanamwabudu Nyerere kuliko yeye na ameamua kumchukua ili wajue kuwa wanaweza pasipo Nyerere.Tena Yeye Mungu pekee ndiye Baba wa vyote. lakini wanadamu wanamwita mwanadamu baba wa taifa? hiyo ni kufuru. Elimu ni nzuri, lakini ile inayotoka kwa Mungu.Hii ya wanadamu mara nyingi inakuwa na kasoro nyingi.na wale waliyo nayo husahau kumtegemea Mungu,na kuitegemea elimu yao ambayo mara nyingi inashindwa kuwatatulia matatizo. Elimu ya madarasani na uongozi ni vitu viwili tofauti lakini wanadamu huvutiwa sana na viongozi waliosoma wanasahau kuwa uongozi unatoka kwa Mungu.Na mara nyingi hawa viongozi waliosoma hawaongozi vizuri. Tuna mifano mingi, lakini Nyerere ni mmoja wa hao viongozi wasomi ambao hawakuongoza vizuri.Hotuba nzuri, maneno ya kushawishi akili na kupendwa na waandishi wa habari siyo cheti cha kiongozi mzuri.Na Nyerere anasifiwa kwa hiyo lakini ukija kwenye matendo ya zile hotuba nzuri hakuna hata kijiji kimoja cha maonyesho kuonyesha kuna msomi mmoja aliyewahi kufikiri kuhusu vijiji vya ujamaa na hiki ni kimoja ya vijiji alivyovianzisha, na watu katika kijiji hiki wanafurahia mawazo ya msomi huyo. Lakini Tanzania nzima hakuna hata kijiji kimoja cha ujamaa kilichobaki kama maonyesho ya mawazo ya msomi Nyerere badala yake Tanzania ni moja kati ya nchi masikini duniani. Na yote hayo ni matunda ya msomi mmoja waliyemwita Mwalimu wa umasikini.Sasa mambo yakiwa hivyo najiuliza kwa nini alipoteza muda kwenda Makerere kupata shahada ya DR. ambayo haikumsaidia kuifanya Tanzania mahali pazuri pa kuishi? Bado nasita katika njia mbili, sijui nimpeleke mtoto wangu Makerere apate shahada kama ya Nyerere ndipo aje agombee uongozi wa Tanzaia, au tumtegemee Mungu atupe kiongozi ambaye ataongoza vizuri hata kama hana karatasi ya chuo kikuu? Na kama Mungu anaweza kutupa kiongozi basi hata mimi niko tayari maana kile ambacho sina ni karatasi ya chuo kikuu tu.na kama Nyerere DR. anaweza kushindwa mambo mengi hivyo, basi nina hakika siwezi kushindwa kama yeye.Kwa Watanzania ni vizuri Nyerere aondoke ili tuwe na mawazo mapya na mbinu mpya za kuikomboa kikweli Tanzania.Hata Musa alipokufa ,Yoshua alifanya makuu kuliko Musa Na Yoshua wa Tanzania ni mimi Faustin S. Munishi |