Yesu: Mpende adui yako

Hakuna adui yako aliye adui kwa asili yake,bali ni adui kwa sababu alikuwa rafiki yako.Na kama alikuwa rafiki yako, basi Yesu anaposema mpende adui yako ana maana umpende rafiki yako wa zamani.

Kwamba ameshakutendea mambo mabaya ambayo wewe hukuyatarajia, hiyo haimsumbui Yesu bado anasema mpende adui yako kwani, aliwahi kukutendea mambo mazuri ambayo pia hukuyatarajia.

Siku wanadamu watakapojifunza kumpenda adui ,dunia itakuwa mahali pazuri sana pa kuishi kwani matatizo mengi yaliyoko duniani yanasababishwa na marafiki walioshindwa kukubaliana kwa mambo fulani yakawafanya kuwa maadui.

Tunayo mifano mingi ya kuweza kujifunza, mmoja wao ni ule wa marafiki wawili Watussi na Wahutu walioishi pamoja kwa muda mrefu katika nchi mbili ndogo za Rwanda na Burundi wakiongea lugha moja Wakioa na kuoana.

Hakuna watu wengi waliojua urafiki wao uliazia wapi, wala matunda yaliyokuwa yakipatikana kutokana na urafiki wao, lakini sasa hivi dunia nzima inatafuta uadui wao uliazia wapi kwani matunda ya uadui wao wameyaona.

Kwa sababu matunda ya uadui yanaiva haraka kuliko yale ya urafiki, pengine ndiyo sababu dunia nzima imeyaona, na kuna hatari ya dunia nzima kulishwa matunda ya uadui wakati yale ya urafiki hawakuyaona wala kuyaonja.

Lakini kabla ulimwengu haujaanza kuyabugia matunda ya uadui wa Watussi na Wahutu, ni vizuri iwaulize wahusika kuwa yako wapi yale matunda ya urafiki wao? maana meza itakuwa nzuri ikiwa imeandaliwa matunda yote mawili.

Dunia itakapofanya hivyo ndipo itakapokuwa ikifanya kitu kinachofaa kwa wakati unaofaa. Kwa maneno mengine dunia itakuwa inawaambia Watussi na Wahutu maneno yale yale aliyosema Yesu “Mpende adui yako”.

Kinyume cha hayo ni kwamba dunia italishwa matunda ya chuki ya uadui wa makabila haya mawili na itakaposhiba, itagawanyika kuwa dunia ya makabila mawili yaani Watussi naWahutu.

Sitaki kuwaza yale yatakayotokea baada ya hayo, maana siyo mazuri na ndiyo maana naandika haya ili hatua zinazostahili zichukuliwe haraka kuiepusha dunia na vita vya makabila mawili. Mwenye macho ya kusoma, asome na aelewe.

Akiongea na gazeti la Injili Mhutu ambaye hakutaka jina lake litajwe alikuwa na haya ya kusema,”Sisi hatuna maneno kabisa hawa jamaa walikuja zamani kwenye nchi yetu tukawakaribisha kumbe wao walikuwa na nia ya kututawala.”Aliongea huku akikodoa macho makubwa mekundu kwa hasira.

“Unajua kwa asili Burundi ilikuwa nchi ya wabantu, na Watussi walikuja na n’gombe wakitokea Sudan babu zetu wakawakaribisha kwa nia nzuri maana walipata maziwa kutoka kwao pamoja na nyama.”

Aliendelea bila kutaja ni mwaka gani Watussi wa kwanza waliingia Burundi

“Mambo yaliendelea vizuri tukawa marafiki, wanatupa n’gombe nasi tunawapa mashamba, tunaoa kwao nao wanaoa kwetu. Maisha yalikuwa mazuri tu pamoja na matatizo madogo madogo ambayo tuliyatatua yakaisha.”

“Lakini miaka ilivyozidi kusonga mbele, wenzetu walianza kutuzidi akili wakawa na maendeleo kuliko sisi, kielimu kiustaarabu wakawa wanatupita pole pole japo wao ni wachache na sisi ni wengi.”

“Mambo yalianza kuharibika wakati Watussi walipoanza kujiingiza kwenye uongozi wa kila kitu na wenyeji tukawa bila kujua tunaongozwa na Watussi. Serikali ni walijaa Watussi, bungeni, majeshi yote wakawa wao ndiyo wametawala.”

“Baadhi ya babu zetu wenye siasa kali, waliona jambo hili si sawa, na wakanza mapambano ya kujikomboa kutoka kwenye kile walichokiita kutawaliwa na wageni.”

“Na kwa sababu tayari hawa jamaa walikuwa wameshatuwahi kwenye vyombo vya dola nikiwa na maana kwamba walikuwa wengi jeshini na polisi, babu zetu wakawa kila mara wanakosa mbinu pamoja na silaha za kuendeshea mapambano yao.”

“Kwa kifupi matatizo yetu na Watussi yalianzia hapo na suluhisho lolote la matatizo yetu, lazima liangalie kwa undani mwanzo wa matatizo yetu.”

“Hatuwachukii watussi, wala hatusemi waondoke warudi kwao, kile tunachosema ni tushiriki utawala kwa kuwa sisi ni wengi tuchukue asilimia sitini ya viti bungeni na wao kwa sababu ni wachache viti arobaini.

“Hilo suala ndilo ambalo Watussi hawataki na kwa sababu wana silaha wamekuwa wakitulazimisha kwa mtutu wa bunduki kukubali kuwa chini ya utawala wao, jambo ambalo na sisi japo hatuna silaha hatutalikubali kamwe.”

Akijibu kama kuna tofauti kati ya Wahutu wa Burundi na wale wa Rwanda, alisema: “Tofauti ni majina ya nchi tu lakini Wahutu ni wale wale na mapambano yao yanafanana.”

“Kwa mfano mauaji ya halaiki yaliyofanywa Rwanda yakaipelekea dunia nzima kulitupia macho suala la Wahutu na watussi, yalisababishwa na kile kile nilichokitaja hapo juu.”

“Kwamba Wahutu wa Rwanda walikuwa wamekubaliana kumaliza tofauti zao huko Arusha na wakati tulipokuwa tukisherehekea kwamba Watussi wa Rwanda wamekubali kushiriki madaraka,Ghafla tukasikia kiongozi wa Wahutu ambaye ndiye aliyekuwa tumaini lao ameuawa.”

“Wahutu walikosa tumaini, wakafanya yale waliyoyafanya si kwamba nayafurahia waliyoyafanya, lakini mwanadamu ukimsukuma ukutani sana matokeo yake mara nyingi hayawi mazuri maana Wahutu waliouawa kabla ya mauaji ya halaiki ni wengi pia.”

Injili ilpotaka kujua nini suluhisho la kudumu, kuhusu mzozo wa Wahutu na Watussi alikuwa na haya yakusema:

“Sisi msimamo wetu ni kuwa tunataka tusameheane na tusahau yaliyopita tukae pamoja tujenge nchi yetu. Kila mtu amheshimu mwenzake kama ndugu na matatizo yetu yatatatuliwa na sisi wenyewe maana tunajuana tulikoanzia ila hatuwezi kukaa pamoja kama hatutawali pamoja.” Mhutu aliyekataa kutajwa jina.

Pamoja na Injili Kulishwa tunda zima la uadui wa makabila haya mawili kutoka kwa moja ya kabila hizo, gazeti letu limekataa kumeza uadui huo mpaka lisikie pia kutoka upande wa kabila hilo lingine la Watussi.

Lakini hata iwe nini hakuna sababu inayotosha kumuunga mkono muuaji awe aliua kwanza au alifanya hivyo baada ya ndugu zake kuuawa.

Na inavyoonekana hapa hakuna mwenye haki hata mmoja, si Mtussi wala Mhutu wote wamepotoka wameoza wote pia. Hakuna mtenda mema, la! hata mmoja,koo lao ni kaburi wazi,kwa ndimi zao wametumia hila, sumu ya fira i chini ya midomo yao

inywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu.Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.

Na kama watakataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu atawaacha wafuate mawazo yao yasiyofaa wamsujudie shetani na kumwabudu ambaye kazi yake ni kuchinja na kuharibu.

Lakini wakikubali kuwa na Mungu katika fahamu zao, wote watatubu dhambi ya uuaji, na Mungu mwenye rehema atawasamehe,maana ni yeye aliyesema usiue.

Tena ni yeye aliyesema njoni kwangu enyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo mizito ya dhambi nami nitawapumzisha. Suluisho la kweli la mzozo huu siyo kutoa sababu zilizowafanya muue,bali ni kutubu, kwani hakuna sababu zinazotosha kumfanya mwanadamu amuue mwanadamu mwenzake.

Na baada ya hayo yote mjifunze kuwachukia marafiki zenu na kuwapenda maadui zenu kwani mkiwachukia marafiki zenu hakutakuwepo na maadui wa kupenda ikiwa kupenda ni tatizo kwenu.

na kwa sababu maadui zako wote walikuwa marafiki zako, ndiyo maana Yesu akasema, “Mpende adui yako”. Kwa maneno mengine mpende rafiki yako wa awali.Alikuwa rafiki yako akawa adui, ukimpenda atakuwa rafiki wa kweli.

Toleo lijalo la Injili, litakuletea mahojiano na Mtussi .
Na mwandishi wa Injili Munishi

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>