Kilio cha mnyonge

Na itakuwa kwamba wewe uliye na mamlaka katika shirika la umeme tena mtu hapati umeme bila wewe.Na amekuja kwako mtu anaehitaji huduma ya umeme usimshughulikie kwa sababu hana chai ya kuweka mbele yako.Basi ataondoka mnyonge mbele yako, akalie kwa Mungu wake.Ujue hakika kilio chake kitasikiwa na yatakayokupata Mungu anajua. Pesa zote unazowanyan'ganya watu, nawe utanyang'nywa kwa njia moja ama ile nyingine.

Na wewe mwenye mamlaka ya kuwapa watu haki za kisheria. Tena mtu haingii Korokoroni bila ya amri yako, na amekuja mnyonge kwako ambaye anashtakiwa uongo na Mtesi wake. Na hukumu yako ikampendelea Mtesi kwa sababu amekupa Pesa alizowaibia watu.Itakuwa kwamba mnyonge atakapokuwa jela, atamlilia Muumba wake. Hakika janga kubwa litakupata kabla ya kumaliza zile pesa ulizopewa.

Amekuja kwako mnyonge anakutaka uandike kisa chake gazetini, unamfukuza kwa sababu gazeti lako limejaa visa vya wale wanaokulipa. Ndipo atakapoondoka mbele za uso wako na amlilie Mungu. Kama hutafutwa kazi, basi gari uliyonunuliwa na wale unaowaandika kila siku kwenye gazeti, litafanya ajali na kufa hutakufa. bali utaishi kwa mateso mengi.

Itakuwa kwamba wewe Tingo wa matatu au dala-dala wanavyoziita Tanzania, mnyonge ameingia ili asafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine. Na wewe ukamtoza nauli ya safari nzima, kumbe mnyonge alikuwa amebakiza pesa ya unga, na wewe umeichukua. Hakika watoto wa mnyonge wakilala njaa. watamlilia Mungu. na kesho wembe ule ule ulioutumia kumnyoa mnyonge utatumika kukunyoa wewe. Polisi wa usalama barabarani watakusimamisha bila sababu, na watadai elfu tatu kwako. Sasa ni mawili, utoe, au ulale kwenye kile chumba chenye mbu na chawa wanaomuuma mtu utadhani wanalipwa mshahara kwa kazi hiyo.

Ulimsukuma Mnyonge, na wewe sasa unasukumwa. kwa maana maisha ni kusukumana.

Nyumba siyo meno, kila mtu awe nayo. Na hata meno mtu hazaliwi nayo. Na wewe mwenye nyumba umesahau. ndiyo maana umemtupia mnyonge vitu vyake nje, kwa sababu unataka kupandisha bei ambayo mnyonge hataiweza. Ole wako maana, Benki iliyokukopesha nayo itashindwa kukuvumilia wakati utakapotoka Hospitalini, kutibu majeraha uliyoyapata baada ya kuvamiwa na majambazi. Na yote hayo yasingekupata kama si kilio cha mnyonge kwa Mungu wake.

Mbona unashangaa, mkuki kwa nguruwe sawa. lakini kwako ni wa uchungu siyo? Unasahau ulipokuwa mkuu wa mkoa ulimfukuza mnyonge kwenye ofisi yako alipokuwa amekuja kukuomba kibali cha kuhubiri? Mwosha huoshwa. sasa ni zamu yako kulia, na sijui utamllia nani na Mungu ulisema huna habari naye. Lakini yeye ni mwenye huruma ukimwamini atakusamehe na ukimlilia kama mnyonge, atakufariji wakati huu wa mateso yako.

Itakuwa kwamba wewe mwenye madaraka katika ofisi ya Posta, yaani mtu hapati simu mpaka wewe ukubali. Japo akiisha kuipata siyo bure atalipa kila mwezi. Na mnyonge mlimpa moja baada ya maombi ya miaka mitatu. Lakini kila mwezi mnyonge anapokea karatasi ikimtaka alipe simu za ulaya, na wakati hata zile za hapa Huzipiga kwa nadra sana. Imembidi akae bila simu.Akiwa amejiinamia kwa huzuni alimlilia Muumba wake.

Mungu amemsikia na Shirika lenu limebinafsishwa. sasa ukiomba simu asubuhi jioni wanakuwekea. hiyo ni hapa Dar es salaam. Na kwa wale wa mikoani inachukua siku mbili kama imechelewa sana. Na habari nilizo nazo ni kwamba kibarua kiliota majani. Kwani hawa wa sasa wanatumia mitambo ya Kompyuta ambayo wewe hujui kuitumia.

Ndiyo mnyonge hajawahi kwenda ng'ambo, na sijui kama siku moja ataenda. Lakini mjukuu wake alikuja Ofisini mwako ili umpe hati ya kusafiria ukamnyima. Walimlilia Mungu Pamoja, na ninasikia yule mtoto wako ni mlevi wa madawa ya kulevya. hata shule aliacha. Mjukuu haendi, Mtoto wako naye haendi.

Kahawa analima Mnyonge lakini inakouzwa hajui. na wewe una madaraka katika chama cha ushirika K.N.C.U. Kahawa yote ya Kilimanjaro inapitia kwako na wewe unaiuza ng'mbo kwa Dola na mnyonge unamlipa kwa shilingi. Katikati ya shilingi na dola, unamwibia mnyonge kwa sababu madarasa hana. Baada ya uchovu wa kazi nyingi kwenye shamba lake la kahawa, anamlilia Mungu. Ndiyo maana nasikia una ugonjwa wa mafuta kuvimbiana tumboni na unahema mara mia tano kwa nusu dakika. Na bado usipotubu, mambo yako sijui yatakuwaje.

Na sasa ni wewe ambaye huna madaraka popote lakini ni mwizi wa magari kwa kutumia silaha. Juzi nasikia ulikwenda polisi kutoa taarifa ya wizi ulofanyika nyumbani kwako. Kinyozi hajinyoi, lakini safari hii? Vinyozi wenzako wamekunyoa. Kwa maoni yangu mnyonge ni kwamba, hawakuiba bali walisogeza vitu ulivyoviiba kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Cha ajabu ni kwamba imekuuma sana. Ajabu!! Na wenyewe watasemaje? Nina neno moja kwako. Tangu umeiba faida gani umepata? Hata viatu umeshindwa kununua, na utakapoiba pesa za kununulia viatu,utakuwa huna miguu ya kuvalia viatu, maana itakuwa imekatwa na risasi.

"Ya Kaisari mpe kaisari "alisema Yesu. Lakini wewe umezidi maana wanaostahili kutozwa kodi huwatozi na wanyonge unawanyanyasa. na watakapomlilia Mungu wao, yaliyowapata wenzako na wewe yatakupata. Usinitishe na gari kubwa hiyo hainibabaishi kwa sababu najua umeipataje. Nausipojirekebisha, hiyo ndiyo itakayokumaliza.

Itakuwa kwamba Mambo yote mazuri au mabaya utakayowatendea wenzako, nawe utatendewa hivyo. Kwani Yesu alisema, Watendeeni watu yale mngependa kuendewa na wao.

Imetayarishwa na Mnyonge.

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>