Munishi Aanzisha Gazeti Jipya la Injili.

Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za Injili Munishi Faustin, ni Mtu mwenye vipawa vingi, kama sanaa inavyohusika.

Munishi alianza kama mchoraji wa picha halafu akawa mhubiri na mwimbaji, na sasa ni mwandishi wa gazeti la Injili. Yote ni sanaa.

“Vipawa unazaliwa navyo mara nyingine unakuwa mtu mzima bila kujua kama unavyo. Na unaweza kufa bila kugundua vipawa vyako vyote. Namshukuru Mungu nimegundua hivi vichache na pengine mambo bado. Ninaendelea kujisikiliza pengine bado kuna vingine nani ajuae.” Alikiri Munishi.

Pengine kuna ukweli kwenye maneno yake maana, Kwa mtu ambaye alimaliza shule ya msingi 1974 na wala cheti cha kumaliza darasa la saba hana, sijui maisha yangekuwaje kama siyo sanaa. Japo yeye anasisitiza ni Mungu ndiye aliyefanya hayo yote baada ya Kuokoka mwaka 1980 huko Arusha Tanzania.

“Unajua nilipokuwa mdogo, nilipenda kuchora picha na kuimba kwenye kwaya ya shule, lakini kwamba siku moja nitakuwa mwimbaji wa kimataifa, wala sikuwahi kuota ndoto. Kila kitu kwangu kilianza mwaka 1980 nilipoamua kumpa yesu maisha yangu, nikazaliwa mara ya pili.” Aliendelea Munishi.

Alizaliwa mwaka 1960 huko Moshi Tanzania . Alianza kuchora mwaka 1975 Jijini Dar es salaam, mpaka 1979 alipohamia Arusha. Ni wakati akiwa Arusha akisukumana na maisha ya ujana ndipo alipoamua kuokoka; Japo tangu mwanzo alikuwa Mkatoliki aliyebatizwa utotoni na kupewa jina la Faustin ambalo anadai hajui maana yake.

“Jina langu hasa ni Ndeyanka Munishi. Hilo ndilo nililopewa baada yakuzaliwa. Ndeyanka ikiwa na maana ya Baba yake mama, au kila mtoto wa pili wa kiume kwa mama Yake. Na Munishi ikiwa na maana ya mwenye nchi. Hili la Faustin nataka kulibadilisha.” Alifoka Munishi.

Hilo la majina halikunisisimua sana kama aliponifugulia Kompyuta yake kunionyesha gazeti lake jipya liitwalo Injili ambalo ameanza kuliandika mwezi wa tisa mwaka 1998. Na kwa sababu uandishi ni kazi yangu, niliangalia pengine nitoe makosa, lakini kinyume chake nilivutiwa na mbinu zake za uandishi.

“Naandika kwa Kiswahili siyo kwa sababu nataka kukijenga kiswahili kuliko wasomi, Bali ndiyo lugha pekee ninayoilewa japo si sana; Lakini naweza kuwasiliana nayo. Sijuti kwa nini sijui Kiingereza bali nafurahi kwa sababu kingeniaharibia huu mtiririko wa maneno ya kiswahili nilio nao.” Alikiri tena.

Niligundua kipawa kingine ndani ya Munishi. Nacho ni kile cha kushawishi. Unapoongea naye usipochunga utajikuta unakubali kila kitu. Ilinibidi nimuulize kama hajui Kiingereza anawezaje kuitumia kompyuta ambayo haiamriwi Kiswahili? maana alivyokuwa akiiamuru utafikiri ndiye aliyeitengeneza.

“Hii yangu nimeweka Kamusi ya Kiswahili ndani, kwa hiyo tunaelewana. Mwanzoni tulikuwa hatuelewani maana, nikiiambia iniangalilie matamshi ya maneno ya kiswahili, ingeniambia kila kitu ni [error] yaani hakuna maneno kama hayo duniani. Lakini sasa inaongea Kiswahili.” Munishi alijitetea.

Nilipoyasoma maoni ya gazeti lake, ilikuwa kama nafasi ya kusoma nyimbo zake. maana jinsi anavyojieleza kwenye nyimbo, ndivyo anavyofanya kwenye gazeti; tofauti ni kwamba akiandika, anajieleza kwa undani zaidi. Yeye ni mhariri mwandishi na ripota wa gazeti lake; Tena ndiye muuzaji na mpiga picha.

“Sijaacha kuimba na wala sitaacha; Na uandishi hauniharibii kuimba kinyume chake unanisaidia . Huwezi kuimba ushindwe kuandika yale unayoyaimba. Lengo langu ni kuwasiliana na watu wengi iwezekanavyo, kuwahubiria maneno ya Mungu. Wamwamini Yesu ambaye ni mambo yote.” Alimaliza Munishi.

Imeandikwa na Mwandishi wetu Ndeyanka.

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>