Media Kenya naTanzania nani bora

Ukipanda juu ya mti kukata matawi, huwezi kufanya kosa ukate lile tawi ulilosimama juu yake. Ukifanya hivyo, wewe na tawi mtajikuta chini. Kwenye makala haya lazima nitafute pa kusimama kwani nitakata matawi yote.

Kama mkata matawi wa kweli siwezi kukata matawi huku nikiwa nimesimamia kwenye matawi hayo hayo.

Vyombo vya habari vinafanana sana na huyo anayekata matawi ya mti. Matawi ni maovu, na mti ni jamii. huwezi kuondoa maovu huku ukisaidiwa na uovu kusimama, maana lazima uache uovu tegemezi ili usimame juu yake.

Mbali na tuhuma za rushwa wanazotupiwa waandishi wa habari, kuna mengi mazuri ambayo yanatakiwa kupongezwa. Kazi nzuri wanayoifanya ya kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha. Wako waandishi wa habari wengi wanaofanya kazi zao vizuri tu bila upendeleo, na hatuwezi kuwacha kuwasifu hawa kwa sababu wachache wameenda kinyume na maadili taaluma yao.

Tangu uhuru Tanzania imekuwa ikitawaliwa na Redio Tanzania na magazeti ya chama na serikali yaani Uhuru na Mzalendo ya kiswahili, na Daily news la kiingereza. Kenya nayo Redio iliyojulikana kama VOK na ambayo kwa sasa ni KBC pamojaja na magazeti kama vile Nation na Standard ndiyo yaliyokuwa na mpaka sasa yanaendelea kuutawala uwanja wa Media Kenya. Tangu wakati huo tumepita kwenye mabadiliko mengi ya kiuchumi kisiasa na kijamii. vyombo vya habari vya Kenya vimekuwa vikibadilika na wakati haraka zaidi ukilinganisha na wenzao wa Tanzania ambao bado wako kwenye ukiritimba wautawala wa chama kimoja wakati kila kilichosemwa na viongozi wasiasa kilipewa uzito kwenye vyombo hivyo hata kama hakina uzito unaostahili. Bado magazeti mengi yanatumiwa na chama kinachotawala CCM kuwaponda wote wenye mawazo kinyume na mwenyekiti wao ambaye kwa sasa ni marehemu.

Media Kenya imepiga hatua kubwa, pengine kuwepo kwa vyombo vya habari vya kimataifa Nairobi ndiko kulikochangia kupevuka haraka na kuwaacha wenzao wa Tanzania wakiimba "Kidumu chama cha mapinduzi, zidumu fikra za mwenyekiti wa CCM" na badala ya wasikilizaji au wasomaji na watazamaji wao kuitikia kiitikio ambacho kilipaswa kuwa "zidumu," Wao wanaitikia "Ni ngumu." hivyo ndivyo waandishi wengi wa habari Tanzania wanavyofanya.

Linalokera zaidi ni wakati wale wanamedia wanaopokea rushwa Kenya wanapokea kitu kizito, wenzao Tanzania huambulia kogombea vinywaji na kuiba vijiko kwenye mahoteli makubwa wakati wanapoitwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari.

Hivi majuzi kulikuwa na malalamiko kwenye gazeti la Rai kwamba meneja wa hoteli moja ya kimataifa kwa jina Sheratoni Hotel amewapiga marufuku waandishi kutumia hoteli hiyo kwa kile alichokiita kugombea chakula na vinywaji kana kwamba ndio mara yao ya kwanza kuona chakula. Pia meneja huyo alisikika akilalamika kuhusu kupotea vijiko baada ya kila mkutano na hao jamaa wanaojiita Third Estate. Ni aibu kubwa. Hawa wanaoiba vijiko na kugombea vyakula na vinywaji ndio tunaowategemea kutuletea habari za kuelimisha na kuburudisha bila upendeleo wa aina yeyote. Tena ndio tunaowategemea watuambie nani anafaa kutuongoza na nani hafai, kupitia makala zao ambazo huzitumia ili kuishawishi jamii juu ya jambo fulani kinyume na jingine.

Siyo ajabu kuna watu wanaamini kuwa picha zote tunazoziona mbele ya gazeti ziko pale kwa misingi ya rushwa na siyo misingi ya taaluma. Pia kuna wengine wanauliza kama habari zote tunazopewa ni habari kweli au kuna masilahi ya watu fulani yanalindwa na habari hizo?

Mwandishi mmoja niliyeongea nae kwa misingi ya kutokumtaja gazetini alisema hakuna utakachokiona katika vyombo vya habari kisilipiwe. alisimulia siku moja alipoandika kisa cha mtu fulani na kumpelekea mhariri wake story hiyo akiwa na furaha kuwa kesho yake ingekuwa ukurasa wa mbele ya gazeti. Kwa mshangao mhariri alimuuliza "Has he behaved?" akiwa na maana "Je ameshachota? alipoambiwa bado alisema "To hell." Yaani story iende jehanamu kwenye moto wa milele. Bado wengine wanashirikiana na wenye majumba au magari kuyaibia mashirika ya bima. Uliona lile gari ambalo picha yake ilikuwa kwenye gazeti likiwa limeungua? Vipi kuhusu ile nyumba iliyoungua wakati kamera ya gazeti na TV zilikuwa tayari kuchukua picha? Au unasemaje kuhusu yule mtu aliyekuwa na bima ya maisha na juzi alipotea nyumbani na inasadikiwa aliuawa na majambazi? Hayo na mengine mengi ndiyo yanayodaiwa kufanywa na wanamedia wote, lakini hawa wa TZ wamezidi na wanatakiwa wabihave kidogo.


<<back    Home  Gazeti La Injili   Injili3  Next>>