Maoni ya mhariri

Mkapa unatuaibisha

Kwamba Polisi nchini Tanzania wameanzisha zoezi la kukamata kanda za dini, hizo ni habari mbaya tena za kusikitisha. Inasikitisha zaidi kuona kuwa zoezi hilo linafanywa wakati huu wa uchaguzi mkuu. Hakuna sababu wanayoweza kuitoa kuhalalisha zoezi hilo ambalo vyombo vya habari vimeubandika jina la 'Operesheni waogopeshe waache kusema.

Sisi katika gazeti la Injili tunalaani kitendo hicho kwa nguvu zote. Pamoja kuwa walioadhiriwa ni wasanii wa nyimbo za Injili na hasa msanii maarufu Faustin Munishi, sisi tunaliona hilo kama pigo kubwa kwa vyombo vyote vya habari. Nani ajuae kesho itakuwa zamu ya nani? Lakini jambo moja ambalo waliohusika ilitakiwa walijue ni kwamba, siku hizi ni vigumu kuzuia information isiwafikie watu.

Tunaishi kwenye ulimwengu wa sayansi na Teknologia, na njia za mawasiliano zimekuwa nyingi ukilinganisha na wakati wa Nyerere. Watu walilazimishwa kuisikliza redio Tanzania, na kusoma magazeti ya Uhuru na Mzalendo. Yalitumiwa na chama tawala kuelezea sera zao za ujamaa na kujitegemea, ambazo zilishindwa kabisa na kuiacha Tanzania ikiwa moja ya nchi masikini duniani. Lakini pamoja na kuwa Tanzania sasa ina utitiri wa vyombo vya habari, huwezi kueleza tofauti, Waandishi karibu wote ni wale wale waliotoka redio Tanzania na magazeti yaliyokuwa yakijulikana kama magazeti ya chama na serikali, na ukiritimba wa chama kimoja bado haujawatoka.

Tuna wingi wa vyombo, lakini ujumbe ni mmoja. Ni mpaka tuwe na waandishi wa kizazi kipya ambacho hakijapitishwa jeshini kupigwa msasa wa siasa ya ujamaa, ndipo tunapoweza kusema kuwa tuna uhuru wa vyombo vya habari. Ndiyo maana mageuzi ya kweli Tanzania yatachukua muda kwani wengi wa wasomi tulio nao ni wale wliokuwa hawafikiri. Nyerere akifikiri kwa ajili yao. Na hata kama walifikiri mzee 'haambiliki' asingewaruhusu kutoa mawazo yao hadharani. Yale tunayotaka kusema hapa ni kwamba, kama kweli tunataka mageuzi ya kweli, lazima tuache kabisa kuwategemea wale waliokuwa viongozi wakati wa Nyerere, kwani wanasema 'mbwa mzee hawezi kujifunza mbinu mpya.'

Wanatumia mbinu zilizopitwa na wakati, badala kuinyamazisha hiyo kanda inayodaiwa kuwa ya uchochezi kwa kusema sera za Nyerere za ujamaa zilishindwa kabisa, sasa wameifanya kanda hiyo kuwa maarufu kuliko ilivyokuwa mwanzo. Sasa kila mtu anatamani kuinunua na kuisikiliza. CCM inaendesha shughuli zake kwa mtindo wa zamani wa kikomunisti ambao umepitwa na wakati. Ni mtindo huo ndio unaowafanya watanzania waonekane kuwa walikuwa wakimpenda Nyerere, na kumbe ukweli wa mambo walikuwa wanamuogopa. Wangempendaje mtu aliyewafanyia majaribio ya siasa ya ujamaa ikashindwa na kuwaacha wakiteseka?

Ni ukweli usiopingika kwamba, hata viongozi ndani ya chama tawala walikuwa hawampendi Julius, bali walimwogopa. Nyerere aliwafanya watu wote kuwa wapelelezi. Baba anampeleleza mtoto, na mke anampeleleza mumewe. Na kwenye nchi ambayo kila mtu alikuwa na kazi kumpeleleza mwenzake, hofu ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini ndiyo iliyokuwa inatawala na siyo heshima wala upendo. Tunasikitika kusema kwamba mwaka mmoja baada ya yule waliyemwogopa kufa, bado Mkapa anataka watanzania wamwogope. Lakini watamwogopea nini wakati dola haimwogopi?

<<back      Home   Gazeti La Injili   Injili3   Next>>