BBC CNN SKY, marufuku Afrika

Vyombo vya habari vya nchi zinazoendelea ikiwemo Afrika ya mashariki vimelalamika kwamba vinalazimishwa kuingia kwenye ushindani usio halali na vyombo vya habari vya mataifa yaliyoendelea jambo ambalo limevidhalilisha na kuvifanya vionekane kama kichekesho katika bara la Afrika.

Soko huru pamoja na ubinafsishaji wa masafa ya kutangazia,ukosefu wa pesa pamoja na kutojiamini ndiko kulikochangi kuzorotesha ubora na nguvu ya kubuni ya vyombo vyetu vya habari, jambo ambalo lisipoangaliwa kwa makini,Afrika tutajikuta katika ukoloni wa Sayansi na teknolojia ambao ni mmbaya kuliko ule ukoloni wa kwanza.

Hatuogopi ushindani bali tunataka ushindani wa haki. Kuyaruhusu mashirika kama BBC CNN kushindana na mashirika yetu, ni kama kumpambanisha simba na swala, na kila mtu anajua matokeo yake. Watu wetu wanalazimika kuacha kusikiliza chochote cha Kiafrika na kuaminishwa kuwa habari iliyoko kwenye mashirika hayo ya nje ndiyo habari hata kama ni ya kumsifu Clintoni au Tonny Blair.

Hebu tuache kuzunguka mbuyu tuseme ukweli. Na ukweli ni huu: Kwamba mashirika haya ya nchi za magharibi hayako Afrika kusaidia,bali kulinda maslahi ya nchi zao na kugeuza hoja za kisiasa ili zilingane na matakwa yao, ndio maana habari zinazowavutia sana kutoka Afrika ni zile za maafa njaa, na mageuzi ya kisiasa.

Mabibi na mabwana wa PRESS, yangu ni hayo machache na ushauri wangu kwa serikali za Afrika ni kwamba ziyapige marufuku mara moja mashirika hayo, kwa faida ya vyombo vyetu vya habari. Mwandishi ni mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye anasikia uchungu sana kwa Afrika kutawaliwa tena.

Imeandikwa na F.Munishi. Sasa niko tayari kujibu maswali yenu.


<<back    Home  Gazeti La Injili    Injili3  Next>>