Kanuni ya Imani

  • “Injili”ni gazeti linalohubiri maneno ya Mungu kwa watu wa dini zote na pia kwa wale ambao hawana dini. Gazeti hili huandikwa na kuhaririwa na Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za Injili Munishi F. Munishi.
  • Zifuatazo ni sera au kanuni za gazeti letu “Injili.” Tunaamini ya kwamba Mungu ni mmoja mwenye nafsi tatu yaani Baba Mwana na Roho Mtakatifu. Tena tunaamini kwamba kuna Mbingu na jehanamu kwamba Mbinguni wataingia Watakatifu na jehanamu wenye dhambi.
  • Tunaamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliyetumwa ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi ambao wa kwanza wao ni waandishi na wahariri wa gazeti hili. Kwamba yeyote atakayemwamini Yesu Kristo na kuzitubu dhambi zake ataokolewa na kuwa na hakika ya wokovu akiwa hapa hapa duniani.
  • Pia tunaamini kwamba Yesu akiwa Mungu alizaliwa kama binadamu na Bikira Maria akateswa, akafa akafufuka siku ya tatu kama yanenavyo maandiko, akapaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Baba akituandalia makao, na atarudi tena kutuchukua.
  • Gazeti la “Injili”linaamini kwamba kila mtu ana haki ya kuamini dini anayoitaka, na kwa kuheshimu haki hiyo gazeti hili halitakashifu dini yeyote, bali litamfundisha kila anayetaka imani ya Mungu kwa kupitia kwa Yesu Kristo, na Injili kama ilivyoandikwa katika Biblia msahafu ambao gazeti hili linauamini.
  • Kwa upande wa siasa tunaamini kwamba Injili na siasa ni vitu viwili tofauti ambavyo haviwezi kuchanganywa,kwani Injili ni maneno ya Mungu na siasa ni maneno ya mwanadamu. Vitu hivyo viwili ni kama mafuta na maji havichanganyikani.
  • Isitoshe tunaamini kwamba Mungu alimuumba Mwanaume kwanza na baadaye Mwanamke si kwamba mmoja ni bora kuliko mwingine, lakini makusudi ya Mungu ni kwamba. Mwanamke atabaki kuwa mwanamke, na Mwanaume vivyo hivyo atabaki kuwa Mwanaume.
  • Upande wa sayansi na nishati, Injili inaamini kwamba dunia pamoja vyote vilivyoko ni mali ya Mungu na vilifanyika kama Biblia ianvyosema, na siyo kama wanasayansi wanavyosema.
  • Tena wanadamu wote ni sawa machoni pa Muumba bila kujali rangi Dini au Nishati na utajiri wa nchi fulani. Na kwamba mali zote za dunia hii zitufae sisi sote,siyo wengine wawe wadaiwa na wengine wanaodai kana kwamba mali hizo walizipata kwenye sayari nyingine ambayo haikuumbwa na Mungu Baba yetu sisi sote.
  • Na hii ndiyo imani yetu kwamba dunia itaongozwa na amri kumi za Mungu, na siyo amri kutoka kwa matajiri wa dunia hii ambao utajiri wao mbele za Mungu ni ubatili mtupu. Kwani Utu wa Mtu haupimwi na vitu maana Mtu ndiye hufanya vitu na siyo vitu kumfanya Mtu awe Mtu. Kwa maneno mengine Mtu ni Mtu hata kama hana vitu.
  • Na mwisho tunaamini kwamba imani ya Mungu huja kwa kusikia au kusoma Injili ya neno la Mungu. Na ya shetani pia huja kwa kusikia au kusoma vijigazeti vinavyoandika uongo wa shetani.
  • Dunia imesikia mabaya, ikaamini mabaya na ndio maana inatenda mabaya. Gazeti la Injili linataka dunia isikie maneno ya Mungu, iamini mazuri,na mwisho itende mazuri.

Ni matumaini yetu kuwa gazeti la Injili litakuwa chaguo lako.

Hayo ndiyo maono yetu, mwanzo wa kila kitu huwa mgumu, lakini kwa sababu tumethubutu kuanza tunaamini tutaendelea. Tuombee,na utusaidie kwa hali na mali.

Anwani yetu ni, Injili S.L.P. 11213. Simu 224092 Nairobi Kenya. Na nambari yetu ya Fax ni 224092 Nairobi.Mungu akubariki na tunatarajia kusikia kutoka kwako. Mhariri wa injili Munishi.

<<Back  |   Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>