Imani huja kwa kusikia

Imani ya Mungu huja kwa kusikia neno la Mungu. Na ya shetani nayo huja kwa kusikia neno lake. Magazeti, Redio na Televisheni huubiri maneno ya nani? Ya Mungu au shetani? Msomaji, msikilizaji au mtazamaji huadhiriwa vipi na maneno hayo? na afanye nini?

Najua wewe ni msomaji wa magazeti ndiyo maana unasoma habari hii. Kwamba huwa unasikiliza Redio na kutazama Televisheni hiyo sijui. Lakini hebu nianze na madhara yanayoweza kukupata kama msomaji sugu wa magazeti.

Kwa sababu yale unayosoma ni maneno, madhara ya kwanza ya maneno ni kusababisha imani. Itakuwa nzuri kama maneno ni mazuri, na itakuwa mbaya kama maneno ni mabaya. Swali la kujiuliza ni hili. Magazeti ninayosoma yana maneno mazuri au mabaya? Na kama yamechanganyikana mabaya na mazuri, nawezaje kusoma yale mazuri na kutoyatupia macho yale mabaya?

Wakristo wengi wamejibu maswali hayo haraka haraka bila kuangalia kwa makini undani wake, na wengi wamepoteza imani yao kwa Mungu kabisa. Hawa ni wale waliosema, “Nitasoma kila kitu halafu baadaye nitaamini yale mazuri tu, na yale mabaya sitayaamini. Walidanganyika; Kwani chochote unachokisoma kinaanza kujenga imani wakati unapokisoma.

Kwa hiyo ukisoma mabaya yakazidi yale mazuri uliyoyasoma, matokeo yake ni imani mbaya. Kulingana na yale unayoyasoma hiyo ndio imani yako. Maana imani huja kwa kusikia na kusikia Neno la Mungu. Jambo ni moja, ukitaka kuwa na imani kubwa kwa Mungu, lazima usome maneno mengi ya Mungu.

Kinyume cha hayo ni imani mbaya ya shetani. Hata wewe unajijua ni imani ya nani uliyo nayo, hiyo sina haja ya kukuambia, hata maneno yako yanatuambia.

Kwani Mtu hutoa yale yaliyo moyoni. Hawezi kusema mema ikiwa yale yaliyo moyoni ni mabaya. Basi wana wa Mungu wanadhihirishwa na yale wayasomayo.

Ole wangu nani ataniokoa na utumwa huu wa kusoma magazeti ya kishetani? Yafuatayo ni maoni machache kukusaidia kuondokana na utumwa huo. Kwanza kabisa unatakiwa ujiulize kwa nini unasoma magazeti? Kama huna sababu za kutosha, acha kabisa maana unaweza kuishi bila kusoma magazeti ya kishetani.

Ikiwa huwezi kuacha mara moja, unaweza kuanza kutumia mikono na macho kama silaha za kujilinda na habari mbaya ambazo hutaki kuzisoma. Watu wengi wanajua kununua gazeti, lakini hawajui kutumia mikono yao kugeuza kurasa ambazo hawataki kuzisoma, bali husoma kutoka mwanzo mpaka mwisho.

Tumia mikono yako kuugeuza ukurasa ambao habari zake siyo nzuri. Japo sehemu ya habari utakuwa umeshaisoma hiyo isikusumbue kwani baada ya kusoma zile habari unazozitaka, soma Biblia kuondoa ule uchafu kidogo uloingia. Hakikisha kuwa unasoma Neno la Mungu kila siku.

Vivyo hivyo kuhusu Redio na televisheni, ukitumia mikono yako kuzima wakati vipindi vya kishetani vinapoanza, utakuwa mhariri wa habari unazozipokea. Pamoja na hayo Mkristo anatakiwa atumie muda mwingi kutoa habari, na siyo kupokea tu. Kutoa habari siyo lazima uwe umesomea kazi ya uandishi wa habari.

Sikukatazi kabisa kusoma magazeti, kusikiliza redio au kuona televisheni, lakini nataka ujue kuwa vyombo hivyo mara nyingi shetani anavitumia kuenezea imani yake. Ndiyo maana tunataka mageuzi katika vyombo vya habari vianze sasa vipindi vya maneno ya Mungu, kama sehemu ya utaratibu wa vipindi vyao.

Lakini suluhisho ni sisi kuwa na vyombo vyetu vya habari, hata kama vitakuwa vikitumia nishati {teknolojia} ya kisasa. Maana duniani hakuna usawa katika usambazaji wa habari. Matajiri wa dunia hii wanatumia nishati ya juu kusambaza habari zenye lengo la kuwafanya watu wote wayaamini mawazo yao.

Na sisi tutatumia njia zozote za kusambaza habari, ikiwa ni pamoja na Setilaiti au barabara kuu ya habari { Intaneti } kuhubiri maneno ya Mungu kwa watu wote Ulimwenguni. Nia na sababu ya kufanya hivyo tunayo. Na penye nia pana njia. Na uwezo wa kufanya hivyo tunao, maana kwa Mungu yote yawezekana.

Ni kweli kwamba tumeingia kwenye karne ya sayansi na teknolojia, lakini hii haimaanishi kuwa waumini wa dini tutakaa kimya tungoje kupigwa mabomu ya habari ambayo yanahatarisha imani yetu kwa Mungu.Nayaita mabomu kwa sababu madhara yake ni sawa.

Ebu fikiri kuhusu radio nyingi zinazotangaza Afrika. Pamoja na kwamba Afrika ni bara lenye utamduni wake, lakini cha ajabu ni kwamba vipindi vinavyorushwa na vituo hivyo vya Radio havizingatii maadili ya utamaduni wa Kiafrika. Utaniambia kuwa hiyo ni kazi ya Serikali za Kiafrika kuchuja ni habari gani watu wake waone.Lakini mawazo hayo yamepitwa na wakati kwani kutokana na teknolojia inayotumika kurushia habari ni vigumu kuweza kuzichuja habari zinazowaangukia watu wake kama mabomu kutoka pande zote.

Bila kusahau masharti inayowekewa Afrika kupata mikopo, kutoka mataifa ya magharibi mojawapo ni kubinafsisha masafa ya kutangazia. Na kila mtu anajua kuwa baada ya kubinafsishwa wanaopata nafasi za kwanza ni hao matajiri wa magharibi. ndiyo maana mashirika kama C.N.N.na B.B.C. yanasikika Katika kila kona ya Afrika, hata zile sehemu za mashambani ambapo waafrika wenyewe hawajaweza kuyafikisha matangazo yao.

Hatari yake ni moja. Kwa sababu Waafrika watakuwa wakisikiliza sana habari kutoka nchi za magharibi, watashindwa kufanya maamuzi yao wenyewe kijamii, kiutamaduni, kisiasa bila kuingiliwa na mawazo kutoka nje.Na inavyoonekana ni kwamba mataifa ya magharibi yanatumia vyombo vya habari kuitawala Afrika, na tayari tunatawaliwa.

Mpaka Afrika ikombolewe kutokana na ukoloni wa habari, ndipo tutaapoweza kusema tuko huru. Lakini mambo yalivyo sasa, tumetawaliwa vibaya na tunataka ukombozi wa haraka. Ndiyo maana hatuwangoji wanasiasa watukomboe, safari hii tumeanza mapambano wenyewe.

Tunataka kuwakomboa watu wetu kutoka katika minyororo na utumwa wa kusikiliza, kuona na kusoma habari ambazo haziendi sambamba na maadili ya utamaduni wetu ambao ndiyo dini yetu.Hatuwezi kuutenga utamaduni wa kiafrika na dini. Na imani ya Kikristo inasisitiza kuwa mila na desturi za mwamini ziheshimiwe na watu wote.Waafrika wasilazimishwe kuishi kama Wayahudi na wala wayahudi wasilazimishwe kuishi kama mataifa mengine.

Na kwa sababu dini huenezwa kwa mawasiliano,ndiyo maana tunalia kwamba njia za mawasiliano zilizoko wakati huu hazitumiki kueneza dini hata kidogo.Ukiangalia utaratibu wa vipindi vya Televisheni na Redio utakubaliana na mimi kwani, hauusishi vipindi vya dini.badala yake kila siku kuna vipindi vya michezo, japo hakuna michezo inayochezwa killa siku.

Ninalotaka kusema ni hili, Watayarishaji wa vipindi vya redio na Televisheni wajue kwamba wasikilizaji na watazamaji wao ni Waafrika wenye dini na utamaduni wa kutunza. Na wakati umefika sasa wa kutovumilia chochote kinachoharibu imani yetu katika Mungu, au utamaduni wetu. Pamoja na kwamba tunavihitaji vyombo vya habari kwa namna moja ama nyingine,mahitaji hayo hayatoshi kugharamia hasara itakayoletwa na vyombo hivyo yaani kuukosa uzima wa milele.Na kama tungeulizwa leo tuchague kati ya Magazeti, Redio, Televisheni na uzima wa milele, uchaguzi wetu utakuwa vyombo vya habari vipotelee mbali, ili tuupate uzima wa milele.

Imeandikwa na Munishi wa Munishi.

<<Back  |   Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>