Nuru na giza

Nuru inaitwa Nuru kwa sababu kuna giza. Lau kusingekuwako na giza, Nuru isingeitwa Nuru na nina mashaka kama ingekuwepo kabisa.

kuwepo kwa giza ndiko kulikosababisha kuwepo kwa Nuru, ili ingae gizani. Maisha ya Nuru yanategemea giza na maisha ya giza vile vile yanategemea Nuru. Lakini hawakai pamoja, maana wanafukuzana. Akiingia Nuru giza anakimbia lakini hafi. Nuru akisinzia kidogo giza anaingia tena. Ndivyo basi maisha ya hawa wawili ni kufukuzana.

Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa akifundisha, alitoa mfano akasema: "Ufalme wa mbinguni umefanana na Mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake.Lakini watu walipolala , akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

Akawaambia , adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi wataka twende tuyakusanye? Akasema la; msije mkakusanya magugu na kuzin'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu."

Mfano wa Yesu unatufundisha kuwa magugu na ngano zinaweza kukua pamoja kabla ya mavuno, lakini wakati wa mavuno lazima zitenganishwe.Na sababu kubwa ni kwamba kuna hatari ya kun'goa ngano wakati zikiwa changa kwani hazina tofauti kubwa na magugu.

Pamoja na hatari ya magugu ndani ya ngano, mwenye shamba anaamua ziachwe zikue pamoja mpaka wakati wa mavuno.

Dunia ni shamba. Na Mungu ndiye mkulima wa shamba hilo. Alimtuma Yesu shambani apande mbegu za Wakristo na aweke mbolea ya damu yake. Na watu walipolala akaja adui naye akapanda mbegu za upagani pamoja na dini nyingine nyingi ambazo siyo za Kikrito.

Siku zote wachungaji wa makanisa ya Kikristo wanamsumbua Mungu wanataka kun'goa magugu.

Na Mungu anawaambia wasijaribu kufanya hivyo, kwani wakifanya hivyo wataatarisha maisha ya hao Wakristo wanaodhani wanawatetea.

Kuna ukweli mkubwa kwenye maneno hayo kwani Ukristo ni Ukristo kwa sababu kuna upagani pamoja na dini nyingine. upagani na dini nyingine zikingoewa basi kazi ya ukristo imeisha, na hakuna sababu ya kuwepo kwa ukristo wenyewe.

Ukristo ni Nuru, na upagani ni giza. Hawa wawili ni maadui watakaoendelea kuwa pamoja mpaka siku ya mavuno ambayo hatujui ni lini.Kinachotakiwa ni Wakristo waendelee kuwa wakristo katikati ya upagani au zile dini nyingine, na mawazo kwamba ni mpaka dini nyingine ziondolewe ndipo Wakristo wasimame, yaondolewe kabisa.

Hakuna vita inayopiganwa na upande mmoja. Ili vita viwe vikali lazima kuwepo na mpinzani. na kama hakuna mpinzani na vita imeisha. Ndio maana msimamo wetu kama gazeti la Injili ni kutokuingilia dini nyingine. maana hatuoni kuwepo kwao kuwa tishio kwetu, bali tunafuhia kuwepo kwa dini nyingine maana hiyo ndiyo inayotupa kazi ya kuandika gazeti la Kikristo. Kama zisingekuwepo, gazeti letu lingeitwa kitu kingine.

Dunia nzima inaamini katika kummaliza adui yako ndiyo uwe salama. Na kuna mifano mingi ya kuthibitisha hayo. Wakati wa vita baridi Wamarekani walifikiri wakimmaliza Mrusi basi wataishi kwa amani, na wataitawala dunia ya Mungu ambayo hawakuiumba. Wanasahau kuwa dunia itaongozwa na amri kumi za Mungu na siyo amri kumi za Marekani.

Niseme nini basi; Kwamba baada ya vita baridi bado wana matatizo mengi ya kusuluisha kuliko awali.Wanachotakiwa kujifunza ni, kuishi na adui. Na siyo kuishi naye tu, na kumpenda pia.

Mfano mwingine ni ule wa Watusi na Wahutu kufikiri kuwa, kummaliza mwingine kwenye uso wa nchi ndiko kutakakomfanya atakaebaki kuishi kwa amani.

Dunia hii ina wema na wabaya. Na mtanisamehe nikisema kuwa wabaya ndio wengi. Pamoja na jitiada za wanadamu kukataa kuishi na wabaya, lakini maisha yenyewe yanakataa kwenda bila wabaya. na kama hakuna wabaya hata wazuri hakuna.

Yaangalie magereza ya dunia nzima. Sehemu iliyotengewa wabaya, lakini ukiingia humo utawakuta wazuri walioingizwa humo kimakosa. Tena ukirudi uraiani ambako walitakiwa wawepo wazuri, utashangaa kuwaona wabaya ambao pengine hawajakamatwa na Polisi ambao na wenyewe siyo wazuri wote, au hakuna ushahidi wa kutosha kutoka kwa raia ambao nao siyo wazuri wote. Au Majaji wawe wliamua kumwachia huru baada ya faili lake kupotea kwenye mahakama ambazo hazisimamiwi na malaika, bali ni wanadamu wale wale wabaya na wazuri. Na bila kusahau hata malaika wenyewe siyo wote wazuri.

Ni baada ya Yesu kuuangalia kwa makini mtiririko huu, ndiyo maana alitoa mfano alioutoa. Kwamba wabaya na wazuri wote ni viumbe wa Mungu na hakuna mbaya aliye mbaya kwa asili yake.

Asili ya wanadamu ni Mungu, na mungu alikuwa mzuri tangu mwanzo.Na asili ya ubaya wote ni shetani. Na shetani hakuwa mbaya tangu mwanzo, kwani alikuwa malaika wa nuru.

Kwamba shetani alikuwa nuru na sasa amekuwa giza, Basi Nuru ya kweli haipaswi kuliogopa giza.

kwani wale wanaoenenda gizani sasa, asili yao ni Nuru. Na ni rahisi kuwarudisha katika asili yao ya kwanza.

Na hiyo ni kazi ya nuru. Kuendelea kuishi kwenye dunia yenye giza, na kuwaangazia mwanga wale walio gizani waone mwanga watoke. Maana giza likiondoka, litaondoka na wao.

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>