Amerika waache mara moja kuwanyanyasa raia wa Iraq

Hata wenyewe hawana uzuri wa kutosha kutuonyesha nani mbaya . Na inawezekana wao ndio wabaya zaidi kuliko Sadam hussein.

Mwendawazimu anapofanya sawa sawa na wendawazimu wake, haimshangazi mtu mwenye akili timamu.Kwani angefanya nini zaidi ya kufanya kiwazimu? Lakini mtu tuliyedhania kuwa ana akili timamu anapofanya kitu cha kijinga tena cha kiwendawazimu, ndipo wajinga,werefu pamoja na wendawazimu wanapomshangaa.

Marekani wamefanya kitu cha kijinga na cha kiwendawazimu pale walipoanza kuwashambulia kwa mabomu raia wa Iraq wasio na hatia. Kitendo hicho badala ya kumpunguza nguvu Sadam kimemwongezea nguvu pamoja na marafiki mmoja wao nikiwa ni mimi.

Kwa uchungu nilioupata baada ya kuziona ndege za Marekani zikimimina mabomu Baghdad kwa siku mbili mfululizo bila hata ndege moja ya Iraq kuangusha bomu Washington, ningekuwa na uwezo ningepeleka ndege kulipua Amerika waache kuwaonea Wairaq.

Lakini pamoja na kwamba uwezo sina hiyo haina maana kwamba uchungu wangu pamoja na wale wengine wanaousikia kama mimi utaishia hapa. Hata kama itachukua miaka mia tatu lazima waamerika walipe haya kwa njia moja ama nyingine.

Wasipoacha mara moja kuwashambulia raia wa Iraq, wajue wanajiongezea maadui dunia nzima. Tena wasijidanganye kuwa baada ya uovu huu watawapooza watu kwa misaada ya dola na vitu. Kwani utu wa Mtu kamwe hauwezi kupimwa na vitu.

Imeandikwa na Munishi.

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>