Aliwekwa huru

Hakujua anaumwa nini pamoja na jitiada zote za kujaribu kujua; lakini alijihisi isivyo kawaida.

Yale aliyokuwa akitaka kuyatenda, hakuyatenda bali yale asiyoyataka ndiyo aliyoyatenda.alijua wazi kwamba anamkosea Mungu, lakini hakuwa na la kufanya kwa sababu yote yaliyokuwa yakitendeka yalikuwa nje ya uwezo wake yeye kama mwanadamu. Pamoja na kwamba alikuwa amebatizwa na kupata Sakramenti zote hiyo haikumzuia kutenda dhambi.

Siku moja alipokuwa anasafiri kwenda sehemu za mashambani, alinunua gazeti la Injili, na alipokuwa akisoma aliona maneno yenye kichwa cha habari Yesu anaokoa. Aliyasoma maneno yote yaliyokuwa kwenye hadithi hiyo, na kugundua kuwa alikuwa akiumwa ugonjwa wa dhambi ambao hauna dawa mahali pengine popote pale, isipokuwa kwa Yesu peke yake.

Aligundua kuwa yeye ni mwenye dhambi na kwamba hawezi kijitakasa mwenyewe hata kama angejaribu kufanya hivyo.Tena alifahamu kwamba, Yesu alikuja ulimwenguni kutafuta na kuokoa wote watakaokubali kwa hiari yao kumwamini na kutubu dhambi zao. Mwisho alijijua kuwa alikuwa mtumwa wa dhambi na shetani na kwamba alitaka ukombozi.

Alitubu dhambi zake akamwamini bwana Yesu, naye akamsamehe na kumpa uwezo wa kufanyika Mwana wa Mungu. Huyo alikuwa Ann Ndunga.

Na wewe unasemaje? Unaweza kuwa mtumwa wa mambo mengi hata wewe mwenyewe unajua jinsi shetani alivyokufunga. Unamhitaji Mkombozi akukomboe kutoka katika utumwa wa dhambi na shetani.

Mwite leo naye atakusikia. Tubu naye atakusamehe. Kumbuka kuwa 'Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi, na Yesu alidhihirishwa ili aziondoe dhambi.[1Yohana 3:4-8].Tena ujue kuwa Mungu anawapenda watu wote lakini anazichukia dhambi. Na mwisho uelewe mambo haya: Atakapozihukumu dhambi, wale watakaokutwa nazo wataangamia pamoja nazo na hapo wa kulaumu ni wao wenyewe.

Na Mwandishi wa Injili Munishi.

 Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>