Yesu ni Mungu? |
Kama mwana wa simba ni simba, basi hakuna kosa lolote kwa mtu mwenye akili timamu kusema kuwa “Mwana wa Mungu ni Mungu.” Huu ni ukweli ambao mtu haitajiki kwenda chuo kikuu kuufahamu, maana hata wale ambao hawakubahatika kwenda shule wanaelewa kuwa mtoto wa panya ni panya. Maneno haya yamekuwa yakizua utata usiokuwa na maana kwani wako wengine wasiotaka kusikia Yesu akiitwa Mwana wa Mungu wachilia mbali kumwita yeye ni Mungu. Kwamba wanataka au hawataki hiyo haimbadilishi Yesu, yeye anabaki kuwa mwana wa Mungu aliye hai, tena yeye na Mungu ni kitu kimoja maana ndivyo maandiko Matakatifu yanavyotufundisha. Mtu mmoja anaamini Biblia na yote yaliyoandikwa humo kuwa ni maneno ya Mungu, na mwingine haamini lakini anaamini kitabu kingine, hawa wote wawili wana haki ya kuamini na kuyasema yale wanayoyaamini. Na mimi naamini Biblia na yale ninayosema yameandikwa kwenye Biblia. Kwamba Yesu ni mwana wa Mungu mwenye Uungu unaomfanya awe Mungu. Isitoshe wote watakaomwamini atawapa uwezo wa kufanyika Wana wa Mungu ili wao pia wawe na Uungu wa kuwafanya Miungu. Kwa hiyo kama kauli ya Yesu ni Mungu inakukwaza, vipi kuhusu hii kauli nyingine ambayo nataka kuitamka sasa hivi kwamba,”Hata mimi nilimwamini Yesu akanipa uwezo wa kufanyika Mwana wa Mungu, nami nikawa na Uungu wa kunifanya Mungu? Kwamba kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, na kilichozaliwa kwa Roho ni Roho, mimi pia nimezaliwa kwa mwili nina jinsi ya ubinadamu,na pia nimezaliwa kwa Roho nina jinsi ya Uungu. Kwa hiyo nina jinsia mbili, moja ni ile ya ubinadamu ambayo hata wewe unayo, na ya pili ni ile ya Uungu ambayo kama huna unaweza kuipata sasa hivi kwa kumwamini Bwana Yesu, kutubu dhambi zako zote, ili uzaliwe mara ya pili kwa Roho, usamehewe dhambi na ufanyike Mwana wa Mungu . Baada ya hayo yote kutendeka ndani yako, utakuwa na Uungu wa kukufanya Mungu, na Kauli ya Yesu ni Mungu haitakusumbua, kwani hata wewe ni Mungu. Kwamba mimi na wewe tunaweza kujiita Miungu, hiyo ni kauli nzito. Lakini pamoja na uzito wa kauli yenyewe, hii haipunguzi ukweli wa kauli,bali ile jinsia yangu ya Ubinadamu inapigana vita na ile jinsia ya Kiungu iliyo ndani yangu kujaribu kunifanya mateka ili niogope kujiita Mungu. Lakini namshukuru Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, kwani kwa kupigwa kwake na kusulubiwa kufa na kufufuka kwake, kumeniwezesha kutoa tamko hili Yesu ni Mungu, bila kuomba masamaha kwa mwanadamu yeyote. Na sitarajii kufanya hivyo baadae. Kwani yale yasiyowezekana kwa mwili, Mungu kwa kumtumia mwana wake Yesu Kristo, alimvika jinsi ya kibinadamu, ili awavishe wanadamu watakaomwamini jinsi ya Kiungu. Kwa hiyo kama yeye alivyovaa mwili akawa mwanadamu,vivyo hivyo sisi tunaomwamini ametuvalisha Roho tukawa Miungu. Kwa sababu Mungu ni Roho, na wamwabuduo imewapasa wamwabudu katika Roho na Kweli. Kwa maneno mengine Mungu alifanyika mwanadamu, ili wanadamu watakaomwamini wafanyike Miungu. Na sasa imekuwa kwamba mtu akiwa ndani ya kristo Yesu ya kale yamepita tazama yamekuwa mapya, yaani utu wa kale umefanywa upya ili yale ambayo tusingeyaweza kimwili kwa sababu ya udhaifu wake, sasa tunawezeshwa na ile nguvu ya Uungu iliyoingizwa ndani yetu kwa imani tuliyo nayo ndani ya Kristo Yesu Bwana wetu, utukufu unayeye milele Amina. Atukuzwe yeye aliyeubeba udhaifu wetu na kutufanya tuyaweze yale ambayo kwa udhaifu wa miili yetu tusingeyaweza. lakini sasa tunaweza kama Paulo mtume kusema “tunayaweza mambo yote katika Yesu anayetutia nguvu. Pamoja na kwamba tumeuvaa mwili, lakini hatuenendi kwa jinsi ya mwili kwani nguvu za Uungu ndani yetu zinautiisha mwili pamoja na tamaa zake. Niseme nini basi, Wokovu ni vita dhidi ya mwili? Ndiyo maana mwili ni wa udongo na roho ni ya Mbinguni. Mwili unatamani ya duniani, na roho inatamani ya mbinguni. kwa kuwa hawa wawili wametofautiana kimalengo, ukiishi kwa kufuata malengo ya mmoja huwezi kumpendeza yule mwingine. Nami nimeamua kuishi kwa kufuata malengo ya Roho wa Mungu ndio maana malengo ya mwili siyatimizi. Ni maombi yangu kuwa ujumbe huu utakusaidia kuamua kuishi kwa Roho ili usizitimize tamaa za mwili maana kufanya hivyo ni mauti, lakini ukiishi kwa Roho ni uzima wa milele. Na mwandishi wa Injili Munishi. |