Haki za Wanaume |
Moja ya haki za wanaume katika jamii ni kuiongoza jamii, na siyo Kuwaachia Wanawake kazi hiyo. Kuwapenda wake zao na siyo kuwapiga. Kutumia nguvu walizopewa kuilinda jamii na siyo kuinyanyasa. Kufanya kazi kwa bidii kuilisha jamii na siyo kuzurura ovyo bila kazi. Wanaume walionyan’ganywa haki hizo wanatakiwa waanze kuzitetea haki zao sasa na siyo baadaye. Hapo mwanzo Mungu alimuumba Mtu wa kwanza. Mwanamume kutoka katika mavumbi na kumpulizia pumzi yake akawa kiumbe hai. Na baadaye aliona si vema huyo Mwanaume akae peke yake, alitwaa ubavu wake akamtengenezea msaidizi yaani Mwanamke. Aliwaweka katika bustani ya Eden ambapo aliwaruhusu kula matunda yote isipokuwa tunda la mti wa katikati. Shetani akitumia umbo la nyoka, alimdanganya mwanamke akala tunda ambalo Mungu alikataza. Siyo kwamba alikula yeye tu, bali alimdanganya na Mwanaume akala pia. Shetani akamdanganya Mwanamke, na mwanamke akamdanganya Mwanaume, dhambi ikaingia ulimwenguni. Ni baada ya dhambi kuingia, ndipo kila mmoja Mwanaume na Mwanamke akapata laana zake ambazo ziliambatana na majukumu ya kila mmoja katika jamii. Ni wakati huo ndipo Mungu aliposema: “Kwa sababu umefanya hayo ewe nyoka, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni, kwa tumbo utakwenda na mavumbi utakula siku zote za maisha yako. Nami nitaweka uadui kati yako na huyo Mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake, huo utakuponda kichwa nawe utamponda kisigino.” Akamwambia Mwanamke: “Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako, kwa utungu utazaa watoto, na tamaa yako itakuwa kwa mumeo,naye atakutawala.” Akamwambia Mwanamume: “Kwa kuwa umeisikiliza sauti
ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza nikisema, usiyale,
ardhi imelaaniwa kwa ajili yako, kwa uchungu utakula mazao yake siku
zote za maisha yako, michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula
mboga za kondeni, kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia
ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa, kwa maana u mavumbi wewe nawe
mavumbini utarudi.” Tangu wakati huo, majukumu ya Mwanaume katika jamii yamekuwa kuingoza jamii huku akifanya kazi ngumu kwa jasho kama alivyoagizwa na Mungu mwenyewe. Tatizo kubwa tulilo nalo siku za leo, ni Wanaume walioyaacha majukumu yao ya kuiongoza jamii, na kuipelekea jamii kubaki bila kiongozi. Wanaume wanaposhindwa kuchukua nafasi zao za uongozi katika jamii, basi matatizo mengi hutokea. Bila shaka matatizo tuliyo nayo leo, mengi kama si yote yamesababishwa na uongozi hafifu katika nyanja zote za maisha. Mwanaume anaposhindwa kukaa na jamii yake nyumbani, na badala yake kupoteza muda mwingi nje ya nyumba yake, matokeo ni nyumba yake inakosa uongozi, na watoto wanaanza kuwa na tabia ambazo hata waalimu hawawezi kuzirekebisha kwani hata waalimu baadhi yao siyo viongozi wazuri wa jamii. Wazazi tena wote wawili wana jukumu kubwa la kuwalea watoto lakini zaidi mzazi kiongozi ambaye ni Mwanaume. Jukumu hilo linapoachiwa waalimu au viongozi wa Dini matokeo yake mara nyingi hayawi mazuri kwani hata viongozi wa Dini siyo wote wazuri. Na kama kazi ya kulea ni ngumu, basi kwa nini mlizaa? hili ni swali langu kwa wale wazazi wanaowaona watoto kama kero. nasema ni kero kwa sababu utawakuta wazazi Mungu amewabariki wana kila kitu wanachokiitaji kuwalea watoto,lakini hawafanyi hivyo. Badala yake wanawapeleka watoto shule za kulala wakiwa bado wadogo, sababu ni eti wanawapenda ndio maana wanafanya hivyo. Lakini uchunguzi uliofanywa na Injili unaonyesha kuwa, siyo upendo unaowafanya wazazi kuwahamisha watoto nyumbani, wakati wanahitaji kujifunza mengi kutoka kwa watu waliowaleta duniani, bali wazazi wengi wanataka ule usumbufu wa watoto uwaondokee, wakae kwa utulivu nyumbani bila kelele za watoto. Na chuki ya watoto siyo kwamba inaanza tu wanapokuwa na umri wa kwenda shule, kwa wazazi wengine chuki hiyo inaanza pale mtoto anapozaliwa, maana tangu akiwa mdogo amekuwa akilelewa na mfanyakazi kwa muda mrefu kuliko na wazazi wake. Utasema alikuwa mdogo hakumbuki. Usidanganyike! anakumbuka yote ndio maana hana uhusiano wa karibu na wazazi. Kwa sababu anajua muda aliokaa na wazazi hautoshi kujenga uhusiano wa karibu na wao badala yake anawaona kama wageni wanaokuja nyumbani kwao usiku na kuondoka asubuhi. Pamoja na uhusiano mdogo ulioko kati yao, bado wazazi wanaamua kumtupia huyo mtoto waalimu ambao na wenyewe ya kwao yamewashinda, na sijui wanamini vipi kwamba watayaweza ya wenzao. Ukweli ni kwamba hawayawezi. ndiyo maana watoto wanaanza tabia mbaya shuleni na wazazi wakitaka kuingilia kati kuwarekebisha wanakuwa wamechelewa, maana samaki usipomkunja akiwa mbichi, akiishakauka hakunjiki tena. Kwanza wanawaona wazazi ni wageni ambao muda mwingi wa maisha yao hawajakaa na wao, Pili wanawaona ni kama watu wa karne ya saba waliopitwa na wakati. Tatu kwa sababu hawakuwahi kupokea amri kutoka kwa wazazi walipokuwa wadogo, hawatakuwa tayari kuzipokea ukubwani. Na wale ambao wazazi walidhani kuwa watawapa amri kwa niaba yao, kumbe amri zao zote hazikuwa zinafuatwa kwani hakuna mtu mkubwa kwa mtoto kama mzazi. Nne tunakuwa na vijana ambao hawapokei amri kutoka kwa yeyote. Na wakati wa likizo wazazi wanajaribu kuwaomba wakae na wao nyumbani, na wao wanasema hawawezi kukaa na wageni wa karne za nyuma, wanatoka kwenda kukaa na watu wa karne ya ishirini na tano, ambayo ni karne ya kuona video zenye picha chafu, pamoja na kusikia miziki ya “Ndom-” Nisimalizie maana na mimi nitakuwa nimesema matusi. Siyo hivyo tu; bali hata nguo zao ni zile zinazopwayapwaya, pamoja na madawa ya kulevya. Na mchezo wa matusi ndiyo chakula chao. Niseme nini? Kusaidika labda Mungu mwenyewe awasaidie, maana hata Makanisa yaliyoko sasa wakienda wanaambiwa watoe ndiyo wabarikiwe na wao hawana cha kutoa labda watoe “bangi’. Lakini Yesu ni yeye jana leo na hata milele. vijana wakitubu watasamehewa. Ndiyo maana ni vigumu kuongea kuhusu haki za Wanaume au Wanawake bila kutaja watoto. Pamoja na kwamba Wanawake wamekuwa na vikao vingi vinavyodai haki zao, kwangu mimi naona wanaume ndiyo wangetakiwa wawe na mikutano mingi ya kudai haki zao lakini cha ajabu ni kwamba hawajafanya hata mmoja. Swali ni kwa nini? ni kwa sababu hawajanyimwa haki zao? au wanajikaza kisabuni? Jibu wanalo wenyewe. Kwa vyovyote vile, wanaume nao wana matatizo yao ambayo wakipata nafasi ya kusema yale ambayo wanawake wanawatendea, utawahurumia. Sasa basi ikiwa Wanawake watakuwa na mkutano wao Beijing wa kuwalaumu Wanaume bila wao kujitetea, na Wanaume nao wawe na mkutano wao Nairobi unaowalaumu Wanawake kwa mabaya wanayowafanyia Wanaume ambayo ndiyo mengi, nani atakuwa mwamuzi? Inavyonekana Mtoto ndiyo anayetakiwa aamue ugomvi huo wakati naye ana matatizo yake yaliyosababishwa na Wanawake na Wanaume. je ataamua? Au ataeleza matatizo yake? Nionavyo mimi Wanawake walikosea kwenda Beijing peke yao na kuwalaumu Wanaume mbele ya watoto. Wangetakiwa kama watu wazima wawaite Wanaume waende wote Beijing, waongee na wamalize tofauti zao. Lakini sasa wameshaharibu maana wameshasema yote, inabidi Wanaume nao waseme yote; ili waamuzi waamue baada ya kusikia kutoka pande zote mbili. Kauli ya wanaume Nayakumbuka maneno niliyoambiwa na babu yangu, nikiwa kijana wa miaka kumi na nane nilipoingizwa Jandoni kwamba; “Mjukuu wangu utakapofikisha umri wa kuoa; jiadhari sana na Mwanamke, kwani anaweza kukuua wakati wowote; Boma ni lako lakini usiingie kimya kimya; kwa nini ufe kabla ya wakati wako? Kohoa kwanza au fanya ishara yeyote kuwaashiria walio ndani kuwa mwenye boma anakuja. Mpe adui nafasi ya kutoroka maana mkikutana kifuani mmoja kati yenu atakufa; Na kwa nini ufe kwa ajili ya asali ambayo huwezi kuimaliza?” Sikuyatilia maanani maneno hayo, lakini miaka ilivyoendelea niliona Wanaume ndiyo wanaokufa kwa wingi kuliko wanawake; Na hata sasa ninapoandika Wanawake waliofiwa na Waume ni wengi kuliko Wanaume waliofiwa na Wake. Kwamba Wanaume wanakufa vifo vya kawaida, au wanawake wana mchango katika vifo vyao, hiyo sijui; Lakini maneno ya Babu sasa nayatilia maanani. Niseme nini juu ya Mwanaume aliyekuwa na mali nyingi na sasa mali zote zimeisha baada ya kudangaywa na Wanawake? Nani amenyimwa haki hapo Mwanaume au Mwanamke? Unakumbuka kisa cha Samsoni na Delila? Wakati delila alipomdanganya Samsoni akasema siri zote mpaka ikasababisha Samsoni kun’golewa macho na Wafilisti; Nani aliyenyimwa haki hapo? Mwanamke au Mwanaume? Muone huyu mwanamke anayewaaribu vijana wadogo wa kiume, akitumia pesa alizomwibia Mumewe, anawafanya watumwa wa kimapenzi pamoja na kuwanyanyasa kijinsia, nani anayenyimwa haki hapa; Mwanume au Mwanamke? Nasema wakati wa kuamka kwenye usingizi umefika; Tumenyanyaswa na Wanawake vya kutosha. Na sasa tunataka mageuzi ya kutufanya tisinyanyaswe tena. Walienda Beijing tukanyamaza, Wakafikiri sisi ni wajinga; Sasa tumejua lengo lao, na hawatafanikiwa. Haki ya kuongoza jamii ni ya Mwanaume, na kamwe hatutawaachia wanawake kazi hiyo. kufanya hivyo tutamkosea Muumba aliyetupa jukumu hilo. Huo ndio msimamo wa Wanaume. Pamoja na kuusikia msimamo wa Wanaume Injili nayo inasema, Matatizo ya Wanawake yamesababishwa na Wanawake wenyewe na yatatatuliwa na wao wenyewe. Kwa hiyo siku nyingine wakiwa na mkutano kama ule wa Beijing, wawaambie wenzao wa kike waache kuwaharibu Waume zao. Vivyo hivyo yale ya Wanaume nayo yatatatuliwa na wao wenyewe. La muhimu ni kwamba, baada ya kelele zote Wanawake watabaki kuwa Wanawake tu. Na Wanaume nao watabaki kuwa viongozi wa jamii tu. Lakini matatizo ya Watoto hayawezi kutatuliwa na wao wenyewe, kwa sababu hawakuyasababisha bali yalisababishwa na Wazazi wa kike na wa kiume. Haya yatatatuliwa na wanawake pamoja na Wanaume bila kuwaacha Watoto. Kwa hiyo mkutano ujao uwe wa Watoto na wazazi wa pande zote mbili. Huu ndio mkutano wa jamii. Na mwandishi wa Injili Munishi. |