Waimbaji na kanisa. |
Kanisa ni mwili wa Yesu Kristo wenye viungo vingi, na kila kiungo hakifanyi kazi moja. Wengine ni Waalimu, wengine Wachungaji, Wainjilisti manabii na wengine wengi. Lakini leo nataka kuzungumzia kuhusu waimbaji wa nyimbo za injili na wachungaji. Mengi yamesemwa kuhusu vita baridi inayoendelea kati ya wachungaji na waimbaji wa nyimbo za Injili, kila upande ukiulaumu ule mwingine. Sitaki kuvichochea vita hivyo, bali kutafuta suluhisho la kudumu la mzozo wenyewe. Wachungaji wachache nilioongea nao, walitoa malalamiko yao kuhusu baadhi ya waimbaji ambao walisema hawaishi sawa sawa na yale wanayoyaimba, jambo ambalo limewafanya wachungaji wengi kukosa imani na waimbaji kabisa. Upande wa waimbaji nao, walikuwa na yao. Wengi wanawaona Wachungaji kama ukuta unaowazuia kufanya huduma ya uimbaji kanisani, na inawalazimu kufanyia huduma hiyo nje ya kanisa. Na mara nyingi huko nje wanakutana na mbwa mwitu wakali wanawararua. Huenda kuna ukweli fulani kwenye maneno yao maana, ukitembea mitaa ya {River Road,} hutakosa kuwaona baadhi ya waimbaji waliojeruhiwa. Lakini cha ajabu ni kwamba hakuna anayekubali kwamba kuraruliwa kwake kunahusika na yeye mwenyewe bali kila niliyeongea naye anasema kuraruliwa kwake kunachangiwa zaidi na Wachungaji ambao wameshindwa kushirikiana na waimbaji na kupelekea waimbaji kulikimbia kanisa. Hata iweje, Kanisa ni la Mungu na sidhani kuna sababu yeyote inayotosha kumwamisha yeyote anayetaka kufanyia huduma ya Mungu kanisani. Tunahitaji kuliangalia kwa upya suala hilo ili shetani asije aklitumia kujenga chuki kati ya makundi haya mawili. Ni kweli inawezekana kuna makosa yanayojitokeza hapa na pale kwenye makundi yote mawili, maana hata wachungaji na wenyewe wana makosa yao. Tofauti ni kwamba mengi ya matatizo ya wachungaji wanajilaumu wenyewe na hapa nina maana ya mchungaji fulani kumlaumu mchungaji mwenzake kwa mataizo yake. Kwamba yamesababishwa na nani, yote ni matatizo na yanataka kutatuliwa. Nionavyo mimi, katiba za makanisa mengi zinachangia kwa namna moja ama nyingine kusababisha matatizo yalioko. Kwanza kipengele kinachomtambua Mchungaji pekee kama mtumishi pekee anayestahili kutunzwa na kanisa, na kuwaacha watumishi wengine ambao pengine wanafanya kazi kubwa na nzuri kuliko ile ya mchungaji bila matunzo yoyote kutoka kanisani. Na inauma zaidi wachungaji wanapopewa magari na kulipiwa nyumba wakati wasanii wanatakiwa wafanye kazi zao kwa misingi ya kujitoea.Na kwa sababu machoni pa Mungu wote ni watumishi. ingependeza zaidi kama kanisa lingewatunza wote. Pamoja na kukosa matunzo, wasanii wanaamua kuwauzia washirika sanaa yao ili na wao waweze kupata riziki kutokana na Injili kupitia sanaa.na hapa nina maana ya kuuza kaseti za nyimbo za Injili au vitabu pamoja na magazeti. Lakini waimbaji wengi niliohojiana nao wanasema kuwa, wanakatazwa kuuza kanda kanisani. Na wale wanaofanya hivyo wanaonekana kama wafanyi biashara kanisani. Au wanakubaliwa kwa masharti kuwa pesa zote zitakuwa mali ya Kanisa, zinunue 'Musso' ya Mchungaji. Ni sababu hizo na nyingine nyingi zinazowafanya waimbaji wa nyimbo za Injili kukimbilia 'River Road' na kuanza kurekodi nyimbo ambazo hazijafanyiwa utafiti na pia hazina ubora kwani zimerekodiwa haraka haraka kwa ukosefu wa pesa za kugharamia Studio. Na baada ya kurekodi mambo hayamalizikii hapo. kwani wanapambana na jiwe lingine kubwa la kuzifanya nyimbo zao zijulikane. Na hapa wanahitaji Televisheni, Redio, na Magazeti. Hapa ndipo wanaporaruliwa na mbwa mwitu wakali, kwani waandishi wengine siyo wote, wanawadai hongo ili habari kuhusu nyimbo zao ziandikwe gazetini. na siyo hao tu kwani hata baathi ya watangazaji wa Redio nao wanataka kitu kidogo ili wimbo usikike kwenye Redio. Bila kuwasahau watayarishaji wa vipindi vya Televisheni {na ieleweke siyo wote} nao wanataka kitu kikubwa ili aonekane akiimba wimbo wake kwenye Televisheni. |