Utu wa Mtu |
Utu wa mtu haupimwi na vitu; Kwani mtu ndiye anaefanya vitu, na wala vitu haviwezi kumfanya Mtu. Mtu hakamilishwi na vitu, Wala hapungui kwa kutokuwa navyo. Mtu ni Mtu hata kama hana vitu. Bwana wetu Yesu Kristo alipopandishwa na Roho nyikani ili ajaribiwe, alifunga siku arobaini mchana na usiku, Mwisho akaona njaa. Mjaribu ambaye ni shetani akamjia akamwambia, “Ukiwa wewe ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kuwa mawe haya yawe mikate.” Naye akajibu akasema, “Imeandikwa Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Mathayo mt. 4: 1-4. Umewahi kupitia karibu na malango ya kuingilia kwa Mtu tajiri, ukiwa umevaa fulana ya mikono mifupi yenye picha kifuani, kofia pamoja na suruale ya jinsi; uone namna mlinzi pamoja na wale walio ndani watakavyokuangalia kwa jicho baya. Unajua ni kwa nini? Wanadhania wewe ni “Mwizi.” Siyo kwamba wana ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa wewe ni mwizi, lakini nguo ulizovaa ndizo zinazowafanya waamini hivyo. na ukifikiri ni mzaha wanaweza kuanza kuita mwizi ! mwizi ! ukajikuta unapigwa kipigo ambacho hata unaweza kupoteza maisha. Jambo la busara ukiona Watu wamekushuku kutokana na nguo ulizovaa, jiondokee pole poole uende ubadili nguo. Kama una koti la mtumba valia, halafu tafuta suruale inayokaribia kufanana na hilo koti wekelea, tena angalia shati lolote lenye vishikizo mpaka shingoni, litupie kifuani. Halafu chukua kitambaa chochote mfano wa kamba, ufunge shingoni. halafu nenda pita pale pale. Cha ajabu utaona ile heshima watakayokupatia. Mara waseme ‘you are very smart,’ Au wanaweza kukuuliza, ‘ Unataka kumwona mzee? Utakapoyaona yote hayo ujue kwamba, wanaheshimu nguo zako na siyo wewe. maana ulipovaa tofauti walikuita mwizi, na sasa umevaa mtumba wanakuita ‘boss.’ Tayari umejua tatizo lao; Ni Watu wanaopima Utu wa Mtu kwa vitu. Wanasahau mwizi ni Mtu na siyo nguo. Tena wanasahau kuwa, nguo hazimfanyi Mtu kuwa au kutokuwa mwizi. Wao wanaangalia vitu vya nje, lakini Mungu huangalia Roho. Maana ndani ya Roho ndiko unakotoka ubaya na uzuri. Shetani alipomuona Yesu ana njaa kali baada ya kufunga siku arobaini, alimwambia ageuze mawe yawe mkate, tena amsujudie ampe vitu vyote. Lakini Yesu hali akijua Utu wa mtu haupimwi na vitu alimjibu kwamba, “Mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila Neno la Mungu”. Tena alimkumbusha shetani kwamba vitu ni vya Mungu, na yeye hana cha kumpa ili amsujudie. Niseme nini kuhusu watu wanaowadharau wenzi wao kwa sababu tu hawana nyumba au hawajafanikiwa kupata gari.Kwao kutokuwa na gari kunakufanya usiwe mtu kamili. Cha ajabu hata Makanisani ubaguzi huu umeingia.Wale wenye vitu vingi vya dunia hii, wanajitenga na waumini wenzao na kusababisha matabaka kanisani.Wenye baiskeli wanakuwa na tabaka yao, maana hata wakitaka kujichanganya na wale wenye magari, wanakuta kuna ukuta mkubwa unaowatenga. Tena inakuwa mbaya zaidi wakati baadhi ya wachungaji wanaonyesha kuwapendelea wale wenye vitu na kuwadharau wale ambao hawana.Tena si hivyo tu, kuna mtindo umeingia siku hizi wa Mapasta kujiona hawajakamilika mpaka wawe na gari aina ya Musso. Wanasahau kuwalenga wenye dhambi wanalenga Musso. na wakiisha kuzipata, wito unaishia hapo.Ndugu zangu watumishi wa Mungu. Mambo hayo hayatakiwi kuwa hivyo.Tumeitwa kwa lengo moja nalo ni kuhubiri injili.Haya ya vitu yasitusumbue. Hakuna haja ya kuwafilisi waumini kwa michango ya kila wiki ili tununue gari za kifahari kama zile wanazoendesha wauzaji wa madawa ya kulevya.Na siyo lazima tufanane na wanasiasa kwani wao huendesha magari makubwa wakidhani yatawafanya wakubwa. Wanasahau kuwa watu wote ni sawa machoni pa Mungu. Hata kama utabebewa nyuma ya [Coast Bus] peke yako, hiyo haikubadilishi badala yake inakuongezea upweke. Na kuna ushahidi wa kutosha kwamba wale wasiyo na vitu vingi, mara nyingi wana utu kuliko wale wenye mali nyingi. Mimi mwenyewe ni shahidi wa mambo hayo,wakati gari langu lilipoungua moto katikati ya barabara. Wenye magari walinipita kana kwamba hakuna kitu cha ajabu kimetokea. Walionisaidi kuzima moto huo ambao ungeniteketeza, ni watembea kwa miguu.Bila kuuliza maswali walianza kuuzima moto na kuyaokoa maisha yangu. Ndiyo maana Mfalme Sulemani alipokuwa akimuomba Mungu alisema, 'Bwana usinipe utajiri nikusahau, wala usinipe umaskini sana mpaka nitamani kuiba mali za watu." Maombi yake yalimaanisha kuwa apate vitu vya kumwezesha kuishi tu.Na siyo vingi mpaka akose kujua hesabu yake. Na akijibu maombi yake Mungu alisema, 'Kwa kuwa hukuomba utajiri basi nitakupa utajiri kuliko Mfalme yeyote duniani." Hii nayo inatufundisha kuomba sawa sawa na mapenzi ya Mungu.Na kwamba utajiri siyo mbaya wakati mtu yuko sawa sawa na Mungu kwani yeye ndiye atakayeusumbua utajiri na wala siyo utajiri kumsumbua yeye. Pamoja na kwamba Sulemani alipotoka baadaye, tatizo lilikuwa kumwacha Mungu, na siyo utajiri.Alipoacha kuyafuata maagizo ya Muumba ndipo matatizo yake yalianza.Kwa hiyo wale wanaoyafuata mapenzi ya Mungu Hata ukiwapa mali za dunia nzima hiyo haiwasumbui.Bado wataheshimu Utu wa Watu wengine. Kwa hiyo utajiri bila kuyafuata maagizo ya Mungu, ni ubatili mtupu na kujilisha upepo.Ndiyo maana matajiri wa dunia hii wasio na Mungu walichokifanya na utajiri wao ni, kutengeneza silaha za hatari na kutumia pesa nyingi kujenga vyombo vya habari kuyasambaza mawazo yao Ulimwenguni, kana kwamba wanadamu wengine duniani hawafikiri. Pamoja na hayo yote, la msingi ni watu wote wajue kuwa Utajiri siyo mbaya. Ila wabaya ni Watu wanaofikiri kwamba unawaongezea kitu katika Utu wao.Wamepotoka; Kwani Utu hauongezwi wala kupunguzwa na chochote. kwa sababu Utu ni Roho, kama vile Mungu alivyo Roho. Mungu haongezwi wala kupunguzwa na chochote kilichoko duniani ama mbinguni. Na sisi aliotuumba kwa mfano wake kwa nini tunakubali kupunguzwa Utu wetu kwa sababu ya vitu? Wakati umefika wa Watu wote kuzisimamia wima haki zao za Utu,kwani Mtu ni Mtu hata kama hana vitu. Na matajiri wa dunia hii nawaonya. Acheni mara moja kutumia utajiri wenu kutengeneza silaha kali, na badala yake mlete hizo pesa tuubirie Injili. Mungu atusaidie tuwapende Watu kwa sababu ni Watu, na siyo kwa sababu ya vitu. Kwani anasema,”Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na hayo mengine mtazidishiwa.” Na mwandishi wa Injili Munishi. |