Tanzania siyo ya Mkapa |
Nchi ya Tanzania ni mali ya watanzania wote na siyo ya Mkapa na CCM kama inavyoekea kuwa.Vitendo vinavyofanywa na serikali ya chama tawala CCM vinaonyesha wazi jinsi wanavyofikiri kuwa Tanzania ni mali yao. Kwamba serikali inaweza kuwaua raia wake kwa sababu wana mawazo yanayotofautiana na chama tawala, siyo tu ni kinyume na haki za binadamu, bali ni wendawazimu uliochanganyika na upumbavu wa hali ya juu. Nauita upumbavu kwa sababu ni afadhali ungekuwa ujinga ambao unaweza kutoka wakati mhusika anapoelimishwa. Lakini kwa kuwa yalifanywa na watu wanaojiita wasomi tena wa vyuo vikuu, basi yanakuwa ya kipumbavu maana hatujui wahusika wataenda chuo gani tena kuelimika ili wajue kuwa katika dunia tunayoishi ni vigumu watu wote kukubaliana kimawazo, hata kama mawazo hayo yanatoka kwa Rais wa nchi. Matata na chokochoko zilizoko duniani mara nyingi huanzishwa na watu wanaojifanya kujua kila kitu, na kumbe hawajui kwamba hawajui. Na Tanzania tuna Mkapa anayejifanya kujua kila kitu na kumbe hajui impasavyo kujua. Matokeo yake ni kwamba Tanzania itaigizwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo havijawahi kuonekana popote duniani. Nasema itakuwa vita mbaya kwa sababu karibu kila mtu Tanzania amepitia mafunzo ya kijeshi, kosa alilolifanya Nyerere akifikiri kila mtu anapokuwa mwanajeshi ni rahisi kumtawala mtu huyo. Jeshini hawaulizi maswali, bali wanatii amri. Ni kigezo hicho ndicho kilichomfanya Nyerere aamini kuwa watanzania wakipata mafunzo ya kijeshi watakuwa na nidhamu, na itakuwa rahisi kuwatawala. Alifanikiwa kuwatawala watanzania kwa karibu miongo miwili bila ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Siyo kwamba Tanzania haikuwa na matatizo, lakini alijua nini cha kufanya yanapojitokeza tofauti na anavyofanya Mkapa ambaye anafikiri kila tatizo linatatuliwa kibabe na kutumia nguvu za dola. Watanzania aliowatawala Nyerere ni wale wale Mkapa anaoshindwa kuwatawala, tofauti ni kwamba Nyerere aliweza kuwaibia watanzania bila wao kujua, wakati Mkapa anawaibia waziwazi. Nyerere alikuwa akigundua wananchi wamemshtukia anawaomba msamaha wa geresha wakati mkapa anamwamuru mkuu wa Polisi awashughulikie wote wanaokuwa na mawazo tofauti na chama tawala. Nao Polisi kama 'Robots' na bila kutumia ubongo wao wanawamiminia risasi za moto ndugu na dada zao watanzania na kusababisha vifo ambavyo idadi yao haitajulikana kamwe. Serikali inasema ni watu 23 tu, wakati chama cha upinzanini CUF ambacho ndicho kilichoadhirika kwa wanachama wake kuuawa kinasema watu zaidi ya 300 waliuawa kinyama na mamia kujeruhiwa huku maelfu wakiwa wakimbizi wa kisiasa Mombasa Kenya kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate uhuru. Na yote hayo yamesababishwa na utawala wa kimabavu wa dikteta Mkapa. Kinachoshangaza na kogopesha siyo idadi ya watu waliokufa, bali tumefikia mahali ambapo Polisi wa Tanzania wanatumia bunduki zilizonunuliwa na watanzania kuwaua watanzania. Mbaya zaidi ni kwamba karibu watanzania wote waliokufa dini yao ni ya Kiislamu jambo linalolielekeza tatizo lenyewe kuwa la kidini zaidi kuliko kisiasa. Siyo kwamba likiwa la kisiasa pekee ni rahisi kulitatua, maana sidhani Tanzania ya leo kuna mwanasiasa anayejua siasa za kutosha kulitatua. Mkapa ni mtoto asiyekua kisiasa na siyo makosa yake. Nyerere baba yake kisiasa hakutaka akue ili awe anamnywesha maziwa ya kisiasa kila siku. Alifikiri angekuwepo mpaka azaliwe mtoto mwingine ambaye naye kama Mkapa, mpango ulikuwa kwamba asiruhusiwe kukua bali aendelee kupewa maziwa ya kisiasa sijui ingekuwa mpaka lini. Lakini alisahau kuwa mwanadamu hawezi kuishi milele duniani, ila mbinguni au motoni ndiko watu wanakoishi milele. Mungu alipoamua kumchuku Nyerere {na sijui alimweka wapi,}Ndipo mambo yalipoanza kumharibikia Mkapa. Kama mtoto yatima kisiasa, hakujua aanzie wapi amalizie wapi. Ninasikitika kusema kuwa mpaka sasa Mkapa amechanganyikiwa kisiasa. Wanaojifanya kumshauri ndio wanaoharibu zaidi. Inavyoonekana hatujui ni nani hasa anaeiongoza Tanzania kati ya Mboma mkuu wa majeshi, Maita mkuu wa Polisi, na Kingunge Nguoyambali Mwiru mshauri mkuu wa Mkapa. Habari kutoka vianzio vyetu zinasema kuna uvutano mkubwa kati hawa watatu kila mmoja akidai kuachiwa urithi wa Tanzania. Mboma anadai kuwa Nyerere alimwambia alinde muungano kwa nguvu zote na akiona kuna hatari ya muungano kuvunjika, Jeshi lichukue madaraka. Kingunge naye anadai kuwa Nyerere alimwambia atumie busara yote kuhakikisha siasa zinaendeshwa bila kumwaga damu ya Watanzania. Naye mkuu wa Polisi anadai kuwa Nyerere alimwambia awafuatilie kwa karibu wanasiasa kuhakikisha kuwa hawaiuzi nchi kwa mabepari wa mataifa ya magharibi. Mkapa naye anadai kuwa Yeye ndiye aliyeachiwa nchi kuhakikisha kuwa siasa ya ujamaa haifutiki Tanzania. Ukiyaangalia madai yao, na uwe kidogo ulimfahamu Nyerere, utakubaliana nao kuwa wote wanasema ukweli. Ni ukweli kwa sababu mwalimu alitaka kuwaona kila siku Butiama wakilalamika kwaba hili halitekelezeki kwa sababu linapingwa na lile. Yaani alihakikisha kuwa la mkapa halitekelezeki kwa sababu linapingwa na Mkuu wa Polisi. Na lile la Mkuu wa majeshi linakwamishwa na KINGUNGE NGUOYAMBALI. Wakati kila mmoja wao alipopeleka malalamiko yake Butiama ndipo Nyerere alipata nafasi ya kuwaonyesha jinsi walivyo wajinga, na inasemekana alikuwa akiwafundisha kama watoto wa Nasari. Ndio maana wote wanamwita mwalimu. Ni kweli alikuwa mwalimu wao. Sasa Mwalimu hayupo, na wanafunzi wake wameanza kuvurunda mambo.Tayari Polisi wamewaua raia zaidi ya 50 wasiyo na hatia kwa madai kuwa walihudhuria mkutano wa kuda haki yao waliyonyanganywa na Serikali. Ni baada ya mauaji hayo ndipo Watanzania wameanza kuhoji hivi Tanzania ni ya nani hasa? Wanajiona kama hawana haki ya kudai chochote katika nchi yao.Wakitafuta wa kulaumu wanamuona Nyerere waliyemwita BABA. Wanaona Nyerere alikosea kuwaachia urithi watu wanne tu na kuwasahau watu milioni karibu 40 kutegemea maamuzi ya watu wanne. Matatizo yanayopikwa Tanzania sasa hivi yana michango mingi iliyochangia kuyafikisha hapo yalipo,Lakini Nyerere pamoja na kwamba ni marehemu hawezi kuepuka lawama.Aliitawala Tanzania kama mali yake, na mawazo yake ndiyo yaliyokuwa sahihi, Na hata kama aliweka Mtu, alihakikisha ni mjinga atakayeketi miguuni pake siku zote kufundishwa. Namkumbuka Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye Nyerere alifikiri ni mjinga, lakini baada ya kutawazwa kuwa Rais wa jamhuri ya muungano, alianza kufanya vitu vyake kama mwanaume anayefikiri. jambo ambalo lilimletea mikwaruzo na huyo aliyekuwa akijifanya kujua kila kitu. Kwa sasa kuna Mkapa anayeitwa Rais wa Tanzania, Lakini nikienda Tanzania nitakutana na mzee Ali Hassan Mwinyi kwani kwangu huyo ndiye mtu aliyethubutu kuwa na mawazo huru wakati wa Nyerere kwenye uongozi wa Nyerere. Mkapa na wenzake wanatakiwa wajue kuwa sasa Nyerere hayuko, na majukumu ya kuiongoza Tanzania lazima yahusishe Watanzania wote. Kiburi kwamba wao ndio walioachiwa nchi waache. Hata huyo wanaedai kuwa aliwaachia Tanzania haikuwa yake. Matatizo ya Zanzibar yatafutiwe uvumbuzi wa haraka unaozingatia haki na siyo ubabe kama serikali inavyojaribu kufanya. Madai ya chama cha CUF kwamba uchaguzi urudiwe na iundwe tume huru, pamoja na kubadilishwa kwa katiba yatiliwe maanani kuinusuru nchi na vita vya kidini ambavyo vinaonyesha kila dalili ya kuanza. Wakristo wasifurahi kwamba serikali ya Mkapa inawazibiti Waislamu, wajue kuwa serikali hiyo hiyo inaweza ikawageukia na wao. Mkapa aache mara moja kuitegemea Amerika kumsadia kutatua tatizo la Tanzania kwani sera za Marekani ni kuwanyanyasa Waislamu duniani kote.Wananchi wa Tanzania wana uhuru wa kuamini dini yeyote na ikiwa Wazanzibar wengi ni waislamu sioni sababu ya wao kuadhibiwa kwa sababu ya dini wanayoiamini. Hata kama wanataka kuuvunja muungano kwa sababu wanazozijua wao, wawe huru kufanya hivyo kwani ni kinyume kuwalazimisha kubaki kwenye muungano ambao hawaoni faida yake. Nyerere alipata sifa duniani kwa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, na Mkapa atapata sifa ya kutenganisha Zanzibar na Tanganyika kuepusha umwagikaji wa damu. Kila kitu kina wakati wake. Wakati wa Nyerere ulikuwa wa kuunganisha, siyo vibaya wakati wa Mkapa ukawa ni wa kutenganisha kwa faida ya walio wengi. Kumuenzi Nyerere siyo kumwaga damu kutetea sera zake ambazo alizitetea bila kumwaga damu. Mwisho ni vizuri Mkapa akajua kwamba yeye siyo Nyerere, na kuna vitu alivyoviweza Nyerere ambavyo yeye haviwezi. Pia asisahau kuwa kizazi alichokitawala Nyerere ni tofauti kabisa na kizazi anachokiongoza. Sura nzuri na maumbile ya Nyerere yalimsaidia kusamehewa haraka na umma, Wakati sura ya kutisha na maumbile ya ajabu ya Mkapa yanamfanya awe mtu asiyesamehewa haraka akikosa. Tayari Mkapa ameshaukosea umma wa Watanzania kwa kuamuru Polisi wawaue zaidi ya watu hamsini huko Zanzibar, sijui itawachukua muda gani kumsamehe. Lakini kama ningekuwa Mkapa, Ningejiuzulu niombe msamaha, halafu niruhusu jeshi lichukue uongozi kwa muda, na baadaye limkabidhi Kijana Faustin Munishi madaraka. |