|
Wakati watanzania wanajiandaa kuingia kwenye uchaguzi wa kwanza
tangu kuaga dunia kwa Julius K. Nyerere, wengi wanauona kama kipimo
kikubwa cha kuona kama watanzania walikuwa kweli wamekomaa kisiasa
au walikuwa wakimwogopa Nyerere na kuficha makucha yao.
Tayari Zanzibar imeshaanza kutoa makucha yao ambayo yanaashiria kuwa wao walikuwa wanaburuzwa na Mwalimu na kamwe waliyokuwa wakiyafanya siyo mapenzi yao kwa Nyerere bali woga waliokuwa nao. Hii inathibitishwa na jinsi wanavyoupinga muungano na tayari wametoa kauli zinazoonyesha kuwa wao wangependa kutawaliwa kidini, na Uislamu ndiyo dini wanayoiona inafaa kufanya kazi hiyo. Nani alijua kama siku moja mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili Faustin Munishi naye angeibuka na kuimba kwamba "CCM dini ya Nyerere imezeeka, sera zake zimeiharibu Tanzania, na ujamaa ulishindwa kabisa." isitoshe kwenye wimbo anamalizia kwa kusema "Msiwarudishe CCM madarakani kabisa." Kwamba naye anadai kutumwa na Mungu kuiongoza Tanzania kwa misingi ya kidini, na dini anayoiona inafaa kufanya kazi hiyo ni Ukristo au dini nyingine yeyote mradi iwe ya Mungu wa kweli, huo ni ushahidi wa kutosha kuwa uchaguzi wa mwaka huu una vimbwanga vya aina yake na hautabiriki. Unakuwa uchaguzi wa aina yake kwa sababu siyo wa vyama vya kisiasa kama tulivyozoea, bali sasa dini imeingizwa kwa nguvu zote na wanataka vyama vya siasa viache kabisa kuutafuta uongozi Tanzania, na badala yake viiachie kazi hiyo Dini itakayomwakilisha Mungu wa kweli. Ugumu unakuja pale kila dini inapodai kuwa yenyewe ndio ya kweli na zile nyingine ni wababaishaji tu. Lakini wengi wanauona huo siyo ugumu hata kidogo kwani hata vyama vya siasa huuza sera kwa wananchi na kwa kufanya hivyo kila chama hujiona bora kuliko kingine. Na kwenye dini vile vile. Yenye Mungu wa kweli ndiyo itakayoongoza, na nyingine zikubali kuongozwa. |