|
Serikali ya Tanzania imepiga marufuku kanda zote za dini zisiuzwe
katika nchi. Pamoja na kwamba hawajatangaza rasmi, lakini wote
wanaokutwa na kanda hizo wanawekwa ndani bila kufikishwa mahakamani.
Polisi wamekuwa wakiwashika wenye maduka ya kanda kwa madai kuwa
wanauza kanda ambazo nyimbo zake haziitukuzi CCM wakati huu tunapokaribia
uchaguzi mkuu.
Kwamba safari hii wanazikamata kanda za dini na kuacha zile za 'NDOMBOLO YA SOLO' ziendelee kuitukana jamii , inaonyesha wazi jinsi mkapa alivyo na uchu wa madaraka mpaka anamsahau Mungu Muumba wake. Nasi waimbaji wa injili tumeamua kwamba hatuwezi kutunga nyimbo za kuisifu CCM tuache kumtukuza Mungu. Mkapa aamue la kutufanya maana dola na silaha zote anazo yeye. Na sisi tunamjia kwa jina la Bwana wa majeshi yote ya mbinguni na duniani.Silaha zetu ni neno la Mungu ambalo ni upanga ukatao kuwili. lakini hatuogopi matisho ya aina yeyote ile. Tumeitwa kumtumikia Mungu na siyo Mkapa. Kama anangoja siku tutakapotunga wimbo wa kumsifu asahau hiyo. Tangu wakati wa Nyerere wasanii pamoja na vyombo vya habari Tanzania hawakuruhusiwa kusema chochote kinyume na chama kinachotawala. Inasadikiwa kuwa utawala uliwabana wasanii kiasi cha kuwanyima studio za kurekodia sanaa yao. Tanzania ina wasanii wazuri ambao hawatambuliwi na serikali yao. Sababu ni kuogopa nguvu ya sanaa isije ikatumiwa kupinga mawazo hasa ya ujamaa siasa ambayo Tanzania iliikumbatia kwa nguvu zote. Wasanii kama Mbaraka Mwinshehe walikufa Kenya wakitafuta mahali pa kurekodia sanaa yao. Ilikuwa ni kama mama aliyekufa akitafuta mahali pa kujifungulia mtoto ambaye siku zake za kuzaliwa zilikuwa zimetimia. Japo Mbaraka hakuwahi kutunga nyimbo kinyume na mawazo ya Nyerere lakini kifo chake serikali ya Tanzania ilihusika kwa namna moja ama nyingine. Kitendo cha Nyerere kukataa makusudi wawekezaji wasijenge studio ya kurekodia sauti Tanzania, kilikuwa hukumu ya kifo kwa wasanii wote wa nchi hiyo. Akijua wazi mawazo yake ya ujamaa yalikuwa na kasoro nyingi, hakutaka kukosolewa na yeyote yule. Vyombo vya habari aliviweka mkononi ili vimsaidie kuhubiri injili yake ya kishetani kwamba watu wahame kwao walikozaliwa wakakae kwenye vijiji vya ujamaa mahali ambapo mtu atakuwa hana chake, ila kila kitu ni chetu hata mke ni wetu! Mawazo ya ajabu sana haya. Niseme nini kuhusu msanii Maneti ambaye aliongoza kundi la Vijana Jazz, jinsi alivyotumiwa na Nyerere kueneza siasa yake mbaya na baadaye alikufa Nairobi baada ya kufunguka macho na kuanza kutunga nyimbo nyingine mbali na zile zilizotarajiwa za siasa. Kwamba vifo vya wasanii wote hao vilitokea baada ya kwenda nchi ambayo Nyerere alikuwa akiita ya mabepari na makabaila bado nina wasiwasi kuwa walikufa kikawaida tu. Redio Tanzania mpaka leo bado nyimbo zinazochezwa huko ni zile zinazosema kuwa kidumu chama cha majambazi, na zidumu vikra za mwenyekiti wa majambazi hao yaani Nyerere. Chuki ya wasanii wenye mawazo huru haikuanza leo ila watoto wanafanya yale waliyomuona baba yao akitenda. "Ndiyo maana waliposema Munishi tutamuua na kuwatisha wenye maduka ya kanda nchi nzima sikulichulia hilo kama mzaha, ilinibidi niagize malaika wengi zaidi kutoka mbinguni kuimarisha ulinzi wa mtumishi wa Mungu. Na tayari nina ulinzi wa kutosha kutoka mbinguni.Wakijaribu wataona moto maana watakuwa wanapambana na Mungu mwenyewe." Sikusema kitu kigeni, wala sikusema uongo kwa sababu nimeimba nikasema "CCM imezeeka, sera zake ni mbovu zimeharibu Tanzania, tena msiwarudishe madarakani kabisa."Ikiwa hiyo tu imewakera kiasi hicho, basi inaonyesha jinsi mlivyokuwa mmezoea ukiritimba wa chama kimoja. Yote niliyoyaimba nimenukuu maneno ya Nyerere mwenyewe aliyesema kuwa ujamaa ulishindwa baada ya kuufanyia majaribio Tanzania kwa miaka zaidi ya ishirini na mitano. Kwani CCM inataka iendelee kutufanyia majaribio hata lini? itupe nafasi ya kupumua maana imetubana kwa miaka mingi na sasa tumechoka. Tunataka uhuru ili tuimbe kile tunachotaka, na tuchague kile tunachotaka.Msitulazimishie CCM maana tunasikia kichefuchefu tutatapika bure. Kwani CCM ni nani? Hata Mungu mwenyewe ametupa uhuru wa kuchagua yale tuyapendayo sembuse CCM chama cha Majambazi? Tulikuwa kimya sasa mmetuchokoza wenyewe na kututishia maisha na silaha. Mnasahau Mungu hawaogopi hata kidogo. |