-
“Injili”ni gazeti linalohubiri maneno ya Mungu
kwa watu wa dini zote na pia kwa wale ambao hawana dini. Gazeti
hili huandikwa na kuhaririwa na Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo
za Injili Munishi F. Munishi.
-
Zifuatazo ni sera au kanuni za gazeti letu “Injili.”
Tunaamini ya kwamba Mungu ni mmoja mwenye nafsi tatu yaani Baba
Mwana na Roho Mtakatifu. Tena tunaamini kwamba kuna Mbingu na jehanamu
kwamba Mbinguni wataingia Watakatifu na jehanamu wenye dhambi.
-
Tunaamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliyetumwa
ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi ambao wa kwanza wao ni waandishi
na wahariri wa gazeti hili. Kwamba yeyote atakayemwamini Yesu Kristo
na kuzitubu dhambi zake ataokolewa na kuwa na hakika ya wokovu akiwa
hapa hapa duniani.
-
Pia tunaamini kwamba Yesu akiwa Mungu alizaliwa
kama binadamu na Bikira Maria akateswa, akafa akafufuka siku ya
tatu kama yanenavyo maandiko, akapaa mbinguni na ameketi mkono wa
kuume wa Baba akituandalia makao, na atarudi tena kutuchukua.
-
Gazeti la “Injili”linaamini kwamba kila mtu ana
haki ya kuamini dini anayoitaka, na kwa kuheshimu haki hiyo gazeti
hili halitakashifu dini yeyote, bali litamfundisha kila anayetaka
imani ya Mungu kwa kupitia kwa Yesu Kristo, na Injili kama ilivyoandikwa
katika Biblia msahafu ambao gazeti hili linauamini.
-
Kwa upande wa siasa tunaamini kwamba Injili na
siasa ni vitu viwili tofauti ambavyo haviwezi kuchanganywa,kwani
Injili ni maneno ya Mungu na siasa ni maneno ya mwanadamu. Vitu
hivyo viwili ni kama mafuta na maji havichanganyikani.
-
Isitoshe tunaamini kwamba Mungu alimuumba Mwanaume
kwanza na baadaye Mwanamke si kwamba mmoja ni bora kuliko mwingine,
lakini makusudi ya Mungu ni kwamba. Mwanamke atabaki kuwa mwanamke,
na Mwanaume vivyo hivyo atabaki kuwa Mwanaume.
-
Upande wa sayansi na nishati, Injili inaamini
kwamba dunia pamoja vyote vilivyoko ni mali ya Mungu na vilifanyika
kama Biblia ianvyosema, na siyo kama wanasayansi wanavyosema.
-
Tena wanadamu wote ni sawa machoni pa Muumba
bila kujali rangi Dini au Nishati na utajiri wa nchi fulani. Na
kwamba mali zote za dunia hii zitufae sisi sote,siyo wengine wawe
wadaiwa na wengine wanaodai kana kwamba mali hizo walizipata kwenye
sayari nyingine ambayo haikuumbwa na Mungu Baba yetu sisi sote.
-
Na hii ndiyo imani yetu kwamba dunia itaongozwa
na amri kumi za Mungu, na siyo amri kutoka kwa matajiri wa dunia
hii ambao utajiri wao mbele za Mungu ni ubatili mtupu. Kwani Utu
wa Mtu haupimwi na vitu maana Mtu ndiye hufanya vitu na siyo vitu
kumfanya Mtu awe Mtu. Kwa maneno mengine Mtu ni Mtu hata kama hana
vitu.
-
Na mwisho tunaamini kwamba imani ya Mungu huja
kwa kusikia au kusoma Injili ya neno la Mungu. Na ya shetani pia
huja kwa kusikia au kusoma vijigazeti vinavyoandika uongo wa shetani.
-
Dunia imesikia mabaya, ikaamini mabaya na ndio
maana inatenda mabaya. Gazeti la Injili linataka dunia isikie maneno
ya Mungu, iamini mazuri,na mwisho itende mazuri.
Ni matumaini yetu kuwa gazeti la Injili litakuwa
chaguo lako.
Hayo ndiyo maono yetu, mwanzo wa kila kitu huwa mgumu,
lakini kwa sababu tumethubutu kuanza tunaamini tutaendelea. Tuombee,na
utusaidie kwa hali na mali.
Anwani yetu ni, Injili S.L.P. 11213. Simu 224092
Nairobi Kenya. Na nambari yetu ya Fax ni 224092 Nairobi.Mungu akubariki
na tunatarajia kusikia kutoka kwako. Mhariri wa injili Munishi.