Vol. 7 ya Munishi yawakera CCM |
Polisi katika mikoa yote ya Tanzania wameanzisha zoezi la kuzikamata kanda zote za mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili Faustin S. Munishi.Wanadai nyimbo hizo zinakikashifu chama tawala CCM. Isitoshe wote wanaokutwa nazo wanapigwa vibaya na kulazwa rumande bila kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka kama yapo. Kosa lao inadaiwa kuwa wanauza kanda ambazo haziitakii CCM ushindi wakati huu wa uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika October 29 mwaka huu. Kanda hiyo ambayo inanunuliwa kama mkate moto ina nyimbo 13 ukiwemo wimbo 'MPENDE ADUI' ambao kulingana na serikali ya Tanzania ndio uliozua balaa. Mwimbaji katika wimbo huo anawataka Watanzania wasiirudishe CCM madarakani kwani chama hicho sasa kimezeeka. Pia wimbo huo unasema kuwa Siasa ya ujamaa aliyoanzisha Nyerere ilishindwa kabisa kufikia malengo yake. Katika kile kinachoonekana kama mbinu ya serikali kujaribu kuwatia hofu wafanyibiashara wa kanda, watafiti wa mambo wameeleza kuwa CCM inameanza kuhaha, hasa ukitilia maanani kuwa huu ndio uchaguzi huru wa kwanza katika nchi ya Tanzania. Chaguzi nyingine zilikuwa zinaburuzwa na Nyerere aliyekuwa anajifanya kujua kila kitu. Kwa mara ya kwanza Tanzania inaingia kwenye uchaguzi bila Julias. Pia wengine wanasema siyo kitu kigeni kwani Nyerere alitumia mbinu hizo hizo kuwazuia wote waliokuwa na mawazo tofauti na yake. Wakati wa utawala wake vyombo vya habari vililazimishwa kuihubiri siasa ya ujamaa. Nyimbo zilizoruhusiwa kusikika ni zile zilizokuwa zinamsifu yeye na siasa yake. Siyo ajabu kusikia Tanzania ilianza kuwa na Televisheni miaka mitatu iliyopita. Zote zilikuwa juhudi za Kambarage kuwazuia Watanzania wasipate Information. Au mtu atalielezaje hili la Tanzania kutokuwa na studio ya kurekodi nyimbo mpaka sasa? Wasanii wa Tanzania hawana mahali pa kurekodia sanaa yao. Siyo kwamba watanzania hawana uwezo wa kununua vifaa vya studio, bali serikali inajua nguvu ya sanaa ndiyo maana juhudi zao zimekuwa kuimaliza sanaa. Isitoshe wasanii wanaojitahidi katika mazingira hayo magumu hawako huru kuitumia sanaa kujieleza. hawakuwa huru wakati wa Nyerere, na hata sasa hawako huru japo taaluma ya Mkapa ni uandishi wa habari. Benjamin angetakiwa awe anajua haki na uhuru wa kusema, na serikali yake inatakiwa iwaheshimu wasanii na siyo kuwanyanyasa. Kwamba serikali inayoongozwa na mwandishi wa habari inahusika kuwakamata na kuwatesa waandishi na wasanii, siyo tu ni makosa makubwa, bali ni kukiuka haki za binadamu. Lakini siyo ajabu kuona kwamba Mkapa haelewi uhuru wa kutoa mawazo maana hata yeye hakuwa huru kutoa mawazo yake. Alikuwa mwandishi wa Nyerere, na sidhani kwamba alikuwa akiandika mawazo yake kinyume na fikra za mwalimu wake. Kwa hiyo kitendo cha serikali kukamata kanda za injili kimewafanya waandishi kuitilia mashaka taaluma ya Mkapa. "Waarabu wanajuana kwa vilemba" ni msemo wa kiswahili. Lakini mkapa siyo mwarabu mwenzetu kwani hajawahi kuvaa kilemba cha uandhishi wa habari, bali alikuwa bomba la kupitishia mawazo ya Nyerere. Kanda hiyo ambayo imesifiwa na wengi kuwa moja ya kanda nzuri aliyowahi kutoa Munishi, ina nyimbo nyingine ambayo inawalenga waandishi wa habari. Munishi anawauliza waandishi kuwa ni nani aliyewaloga mpaka wafikiri kuwa jamii itaishi kwa siasa tu bila injili? Pia aliwaita wanafiki wanaojifanya kuisafisha jamii kumbe wenyewe ni wala rushwa namba moja, hasa wakati wa uchaguzi ukiona story iko ukurasa wa mbele ujue wanasiasa wamechota mshiko au kitu kidogo. Aliwaonya watoe kwanza boriti ndani ya macho yao ndipo waweze kuviona vibanzi kwenye macho ya wengine. Wimbo mwingine unaotia fora ni "MSIABUDU AMERIKA." pamoja na mambo mengine mwimbaji anaonya dhidi ya kuiabudu Amerika badala ya Mungu. pia kuna wimbo unaoionya jamii kuhusu ukimwi. 'Maji yana mdudu' ni wimbo wa mafumbo rahisi kuelewa. Kanda hiyo pia imezungumzia suala sugu la rushwa miongoni mwa nyimbo nyingine nzuri. Tangu kamata kamata ya kanda hiyo ianze, watu wengi na hasa wale ambao walikuwa hawajaisikia wameonyesha hamu kubwa kutaka kuinunua. Sasa imekuwa maarufu hata miongoni mwa watu wa dini nyingine hasa waislamu. Wanaipenda kwa kipengele cha Amerika isiabudiwe. Kwao Amerika ni adui mkubwa wa waislamu duniani. Naye Munishi anasema alikuwa anatoa mawazo yake, na haombi, wala hataomba msamaha kwa serikali ya Mkapa ambayo itatoka kapa. |