Yesu Anaponya.

Kama kuna kitu kinachowasumbua watu duniani ni matatizo ya afya zao. Hata mataifa yaliyoendelea hayajaweza kuwahakikishia raia wao usalama wa afya zao.

Kwa mataifa ya Afrika mambo ndiyo mabaya zaidi kwani kuna uchache wa Mahospitali, Madaktari na Madawa. Umaskini nao ni ukuta mwingine unaowazuia wengi kupata hizo huduma chache za Afya.

Pengine hii inachangiwa na Waafrika wenyewe kutotilia maanani Madawa ya asili, na kuyakumbatia yale ya nchi za magharibi ambayo hawawezi kuyagharamia, na wale wachache wanaoweza, wanajikuta wakitumia madawa ambayo pengine muda wake wa kutumia umeisha, au ni yale yanayofanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza, ambayo adhari zake kwa mwanadamu hazijafaamika bado.

Upo ushahidi wa kutosha kuyatetea maoni yangu. Kwamba katika enzi za mababu zetu kila ugonjwa ulitibiwa na aina fulani ya mti shamba, na walikuwepo watu ambao kazi yao ilikuwa kuyafanyia utafiti madawa hayo. Na kama watafiti hao wangeendelea mpaka leo, tungekuwa na wanasayansi wetu ambao kugundua dawa ya ukimwi lisingekuwa tatizo kwao.

Nisemalo ni hili, Mungu alipomuumba Mwanadamu alimwekea duniani kila aina ya miti kwa matumizi mbalimbali na moja ya matumizi hayo ilikuwa ni dawa. Kwa hiyo duniani kuna dawa za kutibu kila ugonjwa pamoja na ugonjwa hatari wa dhambi, lakini cha ajabu wanadamu bado wanaumwa na hawajui wapate wapi dawa. Kuendelea kuumwa wakati kuna dawa, hilo siyo tatizo la Mungu, ila ni la Mwanadamu.

"Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekeza watubu dhambi zao na kuniomba, Mimi nitasikia kutoka Mbinguni na kuiponya nchi yao." Asema Bwana wa majeshi.

Wanadamu wakitubu na kuomba, ahadi ya Mungu ni kwamba, atawaponya mahali popote walipo. Hii haijalishi kuwa wako Afrika au Marekani. Mungu atatumia miti na utaalamu uliyoko Afrika kuwaponya Waafrika na atafanya hivyo kwa watu wa mabara mengine. Sasa basi hakuna haja ya kuogopa, kwani popote ulipo Mungu atatumia miti na utaalamu wa hapo kukuponya.

Tatizo la Wanadamu ni kufikiri kuwa utaalamu wa bara lingine ni bora kuliko ule wa kwao. Kwa sababu anayeponya ni Mungu, na utaalamu pia unatoka kwake; Basi anaweza kuutumia utaalamu kidogo kuuponya ugonjwa mkubwa, na pia kutumia utaalamu mkubwa kuponya ugonjwa kidogo. Ili wale walio na utaalamu mkubwa wasiwe na la kujisifu.

Kwani adui mkubwa wa Mwanadamu ni maendeleo. Yeye anafikiri anaendelea, kumbe ndiyo amejitengenezea tatizo la kummaliza haraka. Aliyetengeneza ndege ndiye anaehitaji utaalamu wa kutengeneza mahali pa kuiegesha hewani ili irekebishwe inapoharibika. Na yule aliyetengeneza simu za mkono, ndiye anayehitaji hospitali kubwa kutibu kansa ambayo inasababishwa na hizo simu za mkono.

Nataka kusema nini? Kwamba mengi ya magonjwa anayougua mwanadamu leo amejitengenezea mwenyewe? ndiyo. Na hii ndio sababu nchi zenye viwanda vingi, na magonjwa ni mengi kama viwanda vyenyewe. Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake, ndiyo maana mtu naye ni muumbaji wa namna yake. Tatizo ni kwamba Mwanadamu anaumba Gari ,analiendesha akiwa mlevi, anasababisha ajali anaumia, halafu anamlaumu Mungu.

Mungu naye anashangaa !!! "Mimi nimempa uhuru wa kufanya atakavyo, amejitengenezea umeme; Umeme umemchoma ananilaumu? na mimi sijui umeme ni kitu gani, maana siyo moja ya vitu nilivyoviweka ulimwenguni pale mwanzo."

Lakini kwa kuwa Mungu ni mwenye huruma nyingi, bado tukimuomba atuponye anafanya hivyo. Na hatuwezi kumuomba uponyaji wakati hatuamini kuwa yeye anaweza kufanya yale tunayomuomba. Kwanza tunamwamini kupitia kwa Mwana wake Yesu kristo, pili tunamuomba atuponye ugonjwa wowote; na Yeye atatumia njia yeyote kutuponya.

Niseme nini basi? Kwamba Mungu anaweza kuutumia utaalamu wowote uliyoko Duniani kutuponya; Na sifa zisiende kwa wataalamu bali kwa Mungu? Ndiyo! Kwani dunia na vyote vilivyoko ndani yake ni mali ya Mungu. Utukufu una yeye milele na milele amina.

Basi sasa hakuna tofauti ya dawa za kienyeji na zile zinazoitwa za kisasa, kwani Mungu huzitumia zote kuwaponya wanaomuomba na kuzitumia. Na kwa wataalamu wanaowapa watu dawa, wajue siyo wao wanaoponya, bali ni Mungu.

Kwa hiyo waache kuwatoza wagonjwa pesa nyingi.. Nanyi wagonjwa mjue kuwa Mungu anaweza kuutumia utaalamu kidogo uliyoko Afrika kuwaponya. kwa hiyo, siyo lazima kuharibu pesa kutafuta matibabu ngambo kama alivyofanya Mobutu na baadaye akafa tu.

Nakumbuka kisa kimoja kinachomhusu mama yangu mzazi. Alinitembelea Nairobi kutoka sehemu za mashambani nilikozaliwa, na baada ya kukaa siku chache aliugua.

Na kama ilivyo kawaida ya wazee wengi, aliona atapona tu bila kutumia dawa yeyote, lakini mambo hayakuwa hivyo kwake. Kwa sababu alikuwa anaharisha, maji mwilini yalimwishia na tulipomfikisha Hospitalini hali ilikuwa mbaya. Daktari akaamua alazwe.

Mambo yalianzia hapo, kwani kila muuguzi anapokuja kumuuliza habari ya asubuhi, hizo ni shilingi elfu mbili na mia tano, malipo ya salaam za asubuhi bila kuhesabu mchana jioni na usiku.

Baada ya siku tatu Hospitalini tulijikuta tunatakiwa tulipe shilingi elfu arobaini. Kwa mshangao tulitaka tufahamishwe pesa zote hizo ni za nini?

Ndipo tulipopewa orodha ya milo mitatu kwa siku, japo mgonjwa mara nyingi alikuwa akikataa chakula.

Pamoja na elimu yangu ya msingi na n'gumbaru, nilichoweza kuelewa kwenye hiyo orodha ni, Zile salamu za Daktari, na malipo ya chakula asubuhi mchana na jioni. Mengine nilimwita kijana kutoka chuo kikuu, naye akaweza kusoma zile gharama za kupima choo damu, pamoja na kupima ubongo. Nyingine aliniambia kwa lugha ya kisomi kwamba ni [tekniko] sana hata yeye haelewi ni nini

Ilitubidi tulipe elfu arobaini shilingi za Kenya, na tukamwomba Mungu atulinde, janga la kulazwa hospitalini lisije likatufika tena.

Na kila siku tunamshukuru Mungu kwa ulinzi wake maishani mwetu na tunawaombea wale ambao hawajamjua Mungu na uponyaji wake, wamjue sasa. kwani kumjua Yesu ni uzima.

Imeandikwa na F.S. Munishi.

<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>