" Siogopi kwamba Mkapa ataniua, kwani naye atakufa tu" Asema Munishi.

Kufa ni jambo linalompata kila mwanadamu kwa wakati wake. lakini wako wapumbavu wanaofikiri kwamba kumuua mtu anayewapinga kimawazo ni suluhisho. wanasahu kuwa mawazo yakimpata mmoja, kuna mamilioni ya watu ambao wana mawazo sawa na huyu mmoja wanayemuona.

Mkapa na serikali yake walikosea kuwaua watu zaidi ya 50 huko Zanzibar, na wapende wasipende tutasema tu. Munishi ni mmoja kati ya mamilioni wanaoamini hivyo, na kumuua hakubadilishi ukweli huo.

Ndio maana ninapopata barua za matisho ya kuuawa siogopi, bali nawahurumia wauaji kwani ikiwa lengo lao ni kuyauwa mawazo, basi watakuwa na kazi kubwa ya kuua maana wenye mawazo kama hayo tuko wengi.

Walimuua Yesu kwa lengo la kumaliza mawazo yake duniani miaka elfu mbili iliyopita, lakini cha ajabu ni kwamba mawazo yake yako kwa watu wengi kuliko wakati walipomuua Yesu.

Dini misingi yake ni haki kwa watu wote. Hawawezi kuninyamazisha wakati serikali ya CCM inawanyima wananchi wa Tanzania haki ya kutoa mawazo yao. vitisho vya kuniua havinitishi kwani hata wao hawawezi kuishi milele duniani.Wakifanikiwa sana wataweza kuharakisha kile ambacho kingenipata tu.

Nasema wakifanikiwa maana Mungu alimwambia Yusufu amchukue mtoto Yesu pamoja na mama yake wakimbilie Misri, na wakae huko mpaka wakati atakapokufa Herode aliyetaka kumuua Yesu. Mkapa kama 'Herode' anataka kuniua, na Mimi namsikiliza Mungu anasema nikimbilie wapi mpaka wafe waliotaka kuniua.

Maombi yangu kwa Mungu ni kwamba ikiwezekana aharakishe kumwondoa 'Herode' wa sasa ili asifanye mauaji makubwa ya watu wasio na hatia kama yale ya watoto wote wa kiume yaliyofanywa na Herode wa kale. Lakini si kama nipendavyo bali mapenzi yake yatendeke.

Serikali ya CCM ikiongozwa na Mkapa iliwaua watu zaidi ya 50 huko Zanzibar kwa lengo la kuwanyamazisha, ikasahau kwamba damu yao itageuka kuwa mbolea ya mawazo waliokuwa wakiyazuia.Mbaya zaidi ni kwamba wenye mawazo hayo ndani ya CCM ni wengi kuliko wale wa vyama vya upinzani. Japo waliouawa ni Waislamu wasio na hatia, uchungu mwingi kulaani kitendo hicho cha kipumbavu uko kwa Wakristo kuliko Waislamu.

Kadinali Pengo na kanisa lake la Katoliki wanaweza kuwaunga mkono CCM wauaji, lakini wakristo siyo kanisa katoliki pekee. Tena Pengo siyo waumini wote wa Katoliki.Wengi katika kanisa analoliongoza Pengo hawakubaliani na mauaji yaliofanywa na Mkapa japo mwenyewe ni mkatoliki, jambo linaloacha pengo kubwa katika kanisa hilo linaloongozwa kutoka 'Vatican.'

Mungu ni haki, na asili ya mwanadamu ni Mungu, kwa hiyo ni vigumu kumzuia mwanadamu kudai haki ambayo ni asili yake.

Kudai haki hakujui dini au itikadi za kisiasa, bali kunamjua mwanadamu. Ndio maana mwanadamu Mwislamu akinyimwa haki, mwenzake Mkristo atamtetea tena kwa nguvu zote kuliko ambavyo angefanya Mwislamu mwenzake. Ndio maana sio ajabu kwangu kama Mkristo tena niliyezaliwa mara ya pili kwa roho, kuandika makala kama hii ya kuwalaani wauaji kwa nguvu zote.

Mwislamu mwenzangu au Mkristo mwenzangu, haina nguvu kama mwanadamu mwenzangu. Vivyo hivyo mwana CCM mwenzetu au mwana CUF mwenzetu haina uzito wa mwanadamu mwenzetu. Usishangae kusikia CCM chama cha majambazi kimegawanyika mara mbili.

Tayari kuna tetesi kuwa wana CCM wanaoona mbali wameanza kulaani mauaji yaliyofanywa na chama chao.Hawa ni wale wanaowaona wale waliouawa kama wanadamu wenzao, ambao walikuwa na haki ya kuamini waliyoyaamini na kuyasema kwa njia zozote na maandamano ikiwa moja ya njia hizo

Mkapa na serikali yake walifanya upumbavu kuwaua raia wasio na hatia, na sasa wanafanya upumbavu mwingine kuwatishia maisha wanaowasema kuwa walikosea.

Wanadai waliwaua kwa kutotii amri ya serikali iliyojiweka madarakani kinyume na katiba ya nchi. Tena wanataka kila mtu aheshimu katiba ambayo wenyewe ndio wa kwanza kuivunja. Wanawaita wahaini ambao walitaka kuipindua serikali wakitumia visu na mapanga kama silaha. Bado wamewabandika jina la maghaidi wa kimataifa ambao Amerika imeshindwa kupambana nao, na kazi hiyo wamemwachia Mkapa.

Uongo mkubwa na propaganda za CCM. hakuna mwenye akili timamu anayeweza kuyaamini maneno yao. Hata wakisema mpaka moto utokee mdomoni, bado wanabaki kuwa wauaji wanaotakiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuua watu wasio na hatia.

Serikali ya Mkapa inatumia mamilioni ya pesa kutetea makosa kwa kufanya kosa. Inafanya kosa kutumia vyombo vya habari kama TVT Redio Tanzania na magazeti ya Uhuru na Mzalendo kutetea mauaji waliyoyafanya. Vyombo hivyo vimejengwa kwa pesa za wananchi, na vinatumika kuhalalisha mauaji ya wananchi wasio na hatia. Inasikitisha kuona kuwa hata vile vyombo vya habari vya watu binafsi vimeingia kwenye mkumbo wa kukipigia debe chama cha majambazi.Haishangazi kwani lengo lao ni biashara na hawajali wasikilizaji au wasomaji na watazamaji wanapewa habari za kweli au propaganda tu.

Magazeti kama 'Nipashe' 'Mwananchi' na redio nyingi zilizoanzishwa hivi karibuni zina lengo moja tu. Kuhakikisha CCM inaendelea kuwanyanyasa wananchi.Mfanyibiashara kama Mengi anayemiliki ITV na Redio one, pamoja na vyombo vingi vya habari, inasemekana huyo ni CCM damu. Hakuna kosa kuwa mwanachama wa CCM, lakini kuwatumia waandishi wa habari ambao taaluma yao ni kuwapasa wananchi habari za kweli na kuwageuza kuwa wapiga debe wa CCM hiyo ni aibu kubwa kwa wanataaluma hao.

Lakini inafurahisha kuona wananchi wakitumia haki yao kujichagulia magazeti redio na TV za kuangalia. Si hivyo tu, utafiti nilioufanya unaonyesha kwamba mara tu kinapoanza kipindi cha Propaganda za CCM watu wengi kama si wote wanahama kwenda chanel nyingine, au wanabadili mita bendi kama ni Redio.Kwa upande wa magazeti wengi hawasomi kabisa magazeti kama 'Nipashe', 'Mwananchi'na siku hizi 'Majira' kwa kile wanachokiona kama mbinu za magazeti hayo kuipigia debe CCM.

Kitambo gazeti la "Majira " liliheshimika ndani na nje ya Tanzania kwa msimamo wao wa kutetea haki bila kuipendelea serikali, jambo lililopelekea serikali kulifungia gazeti hilo mara kwa mara.

Heshima hiyo sasa imehamia kwenye gazeti la 'Mtanzania' ambalo limesimamia haki hata baada ya mmiliki wake Jenerali Ulimwengu kuvuliwa uraia na serikali ya CCM inayoongozwa na Mkapa aliyekuwa mwandishi pamoja na Ulimwengu kwenye gazeti la 'Daily News' wakati wa Nyerere.

Walitumika wote kama bomba la kupitishia mawazo ya Nyerere, na sasa Mkapa anataka Ulimwengu atumike kama bomba la kupitishia mawazo yake ya kuua, jambo ambalo Ulimwengu amelikataa kata kata.

Wanasema siasa ni mchezo mchafu. Jenerali Ulimwengu. Kwa sasa serikali inasema yeye siyo raia wa Tanzania bali ni raia wa Rwanda. Hawakujua kuwa Jenerali ni Mrundi miaka yote hiyo, mpaka alipowakemea kwa kuwaua watu wasio na hatia huko Zanzibar. Hiyo ndiyo siasa.

Watakubandika kila jina wakati unapowakemea. Tayari mimi wananiita 'Mkosa dini mbumbumbu asiye na elimu, na majina mengi ambayo siwezi kuyataja.' Zote hizo ni propaganda za CCM zenye lengo la kuonyesha kila anayewapinga hafai hata kuishi.

Tuache kutishana, CCM imezeeka haifai kuongoza. Mungu anasema kwamba sasa anataka kuwaongoza Watanzania. Na tayari ameshampaka mafuta ya uongozi kijana Faustin S. Munishi. Kuanzia sasa Mungu ndiye anayeiongoza Tanzania. Wananchi msijali kwamba Mkapa na majeshi yake wako madarakani kimabavu, bali muisikilize sauti ya Mungu inasemaje kupitia kwa mtumishi wake Munishi ambaye amemteua kuikomboa Tanzania.

Vita vyetu siyo vya damu na nyama. Kwa hiyo hatuhitaji jeshi linalotumia AK 47 bali Neno la Mungu. Neno la Mungu ni kali kuliko silaha zote alizo nazo Mkapa. Anatujia na makombora aliyonunua kwa pesa zetu, na sisi tutamwendea kwa jina la Bwana wa Majeshi yote ya duniani na mbinguni.

Kama wana wa Izraeli walivyozunguka kuta za Yeriko mara saba, na wananchi wa Tanzania wanatakiwa kuzunguka Tanzania mara saba. Kila mtu anatakiwa kuzunguka eneo la mahali anapoishi mara saba kila siku kwa muda wa miezi saba tangu anapopata ujumbe huu. Mzunguko huo unatakiwa uanze saa sita ya usiku kila siku, na kila mara ya saba ya kila siku mnatakiwa kutoa sauti ndogo ambayo itaongezeka kadiri siku zinavyokaribia.

Watanzania wote kutoka dini zote, kutoka vyama vyote vya siasa wanakaribishwa katika zoezi hili la kuikomboa nchi yetu. Cha muhimu ni Tanzania izungukwe mara saba.Wakati wote wa kuzunguka, watu wote wanatakiwa kuomba maombi haya: Eee Mungu uliyeangusha kuta za Yeriko, tunakuomba uangushe kuta za CCM na serikali ya Mkapa. Kwa jina la Yesu tumekuomba Amen.

Kwa hiyo wakati wowote kwenye kipindi cha miezi saba kama wazungukaji watakuwa wamemaliza kilomita za mraba kutosha kuizunguka Tanzania mara saba, Kuta za CCM na serikali ya Mkapa zitaanguka. Cha muhimu ni tuwe na umoja na imani moja kamba yale Mungu aliyowafanyia wana wa Izraeli wakati wa Joshua, atatufanyia na sisi wakati huu. Msiogope wala msifadhaike mioyoni mwenu. Vita siyo vyenu ni vya Bwana, kwa hiyo muamini tu.

Msiseme mimi ni Mwislamu au mimi ni Mkristo maana Mungu ameyaona mateso yenu kama wanadamu aliowaumba. Anataka kuwafanyia ukombozi ili baada ya kuuona muujiza wake wa kuangusha kuta za CCM na serikali ya Mkapa inayowatesa na kuwaua watu wasio na hatia, ndipo sifa na shukrani zote mzirudishe kwa Bwana Mungu wenu asiyewajua kwa misingi ya dini zenu, bali kwa imani za nyoyo zenu.

Msiwaogope wanaoweza kuua mwili lakini hawawezi kuua roho, bali mwogopeni na kumsikiliza yule anayeweza kuua vyote viwili mwili na roho yaani Bwana wa Majeshi Mungu muumba wetu. Msitishwe na majina ya kejeli watakayomwita mtumishi aliyepewa jukumu hili, au hila zozote za uongo watakazomtungia ili imani yenu kwake ipungue, bali muwe kitu kimoja ninyi na kiongozi wenu mliyepewa na Mungu. Watafanya kila hila za kishetani, lakini maombi na imani yetu kwa Mungu itamshinda shetani wa CCM pamoja na serikali inayoua.

Ni baada ya ukombozi ndipo Watanzania watakapojua kumbe nchi yetu ni nchi yenye asali na maziwa pamoja na kila aina ya utajiri lakini ibilisi akimtumia Mkapa alitunyanganya mali zetu za asili tulizopewa na Mungu. Tena mtagundua kwamba kwa kuwa kila mtu anamcha Mungu, naye Mungu atayaondoa magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua, maana yeye ni Mungu atuponyae. Isitoshe mtafahamu ya kwamba kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa yote. Watanzania tutabarikiwa na hekima ya hali ya juu kutoka juu, kiasi kwamba hatutahitaji AK47 kwa ajili ya ulinzi mipakani mwetu, bali Mungu atatupa akili ya kutengeneza kitu ambacho hata Amerika hawana.

Sasa hivi Mkapa anadanganywa kwamba ananunua vifaa vya ulinzi, kumbe wanamuuzia vyombo ambavyo wakitaka kuvizima visifanye kazi wanafanya hivyo. Wananchi tunakumbuka wakati Rais Clinton wa Marekani alipotembelea Tanzania hivi karibuni Hakuna chombo chochote cha wana usalama wa Mkapa kilichofanya kazi.inasemekana kwamba mawasiliano yote yalikatwa, na vyombo vya kisasa kutoka Amerika vilitawala anga ya Arusha wakati wote wa ziara hiyo. Hadi Waamerika na Rais wao walipoondoka ndipo 'ova ova' za mashushushu wa mkapa zilipoanza kufanya kazi.Mambo hayatakuwa hivyo baada ya ukombozi. Cha ajabu ni kwamba walisikika wakisema, " Huyo ni Faustin Munishi alikuwa ametuzimia 'OVA'"

 Home |  Gazeti La Injili | Nyimbo Za Munishi