Redio hizi hazifai

Lengo lao siyo kufahamisha kuburudisha na kuelimisha, bali ni kutangaza matangazo ya biashara. Wanawalenga waumini wa dini kibiashara, huku wakiharibu imani zao. Utaratibu wa vipindi vyao hauusishi vipindi vya kidini, bali vipindi ambavyo haviambatani na maadili ya kidini. Wanasema sera zao hazina dini, lakini wanasahau wasikilizaji na watazamaji ni waumini wa dini. Maovu karibu yote duniani, vianzio vyake ni vyombo vya habari.

Lakini mtangazaji mashuhuri wa redio, Ali Salim Mmanga analitetea shirika analolifanyia kazi la KBC, na kusema lawama hizo haziwahusu hata kidogo."Sisi tuna vipindi vya Kiislamu na Kikristo karibu kila siku. "Sijui kuhusu hizi steseni mpya, lakini nasikia watu wakilalamika kuwa zinacheza miziki hasa ile mibaya ya kigeni wakati wote." Maneno hayo yana uzito wa aina yake hasa ukitilia maanani kwamba anayeyasema ni mtangazaji aliyeanza kutangaza tangu mwaka 1976 katika VOK kwa sasa KBC.

Pamoja na kujaribu kuitetea KBC, wengi wanaiona kama haijafanya vya kutosha kuwarithisha wasikilizaji wake, hasa waumini wa dini, kwani vipindi vingi vya kidini ni vile ambavyo wahusika hununua wakati kuvipeperusha hewani. Isitoshe kufanya hivyo malipo yake ni ya juu, jambo linalowafanya wengi washindwe kumudu.

Lakini ukweli unabaki kwamba KBC wanaongoza kuwa na vipindi vingi vya kidini kuliko redio nyingine nyingi zinazojaribu kushindana nao. Ila wanaweza kufanya vizuri zaidi.

Akijibu swali kama ana mpango wa kuihama KBC ajiunge na FM mpya zinazotangaza Nairobi pekee, Mmanga alisema: "Kila siku kwenda usikokujua ukarudi salama ni bahati yake Mwenyezi Mungu. "Siwezi kutoka ninapopajua niende nisikokujua. "KBC inasikika Afrika mashariki na kati, na isitoshe sasa inasikika karibu dunia nzima kutumia mitambo ya setilaiti."Kuiacha nijiunge na vijiredio vinavyotangaza masafa mafupi ya Nairobi pekee, ni kujishushia hadhi yangu, na siko tayari kufanya hivyo."

Hatujui kama msimamo huo atakuwa nao muda gani, maana redio mpya zinatoa mishahara mikubwa, jambo ambalo limekuwa kivutio kikubwa kwa watangazaji wengi kuihama KBC.

Wako watu wanaosema ni heri kuanza redio mpya na watangazaji wapya kuliko kuwaajiri wahamiaji ambao mara nyingi wanakuwa na ukiritimba wa huko walikotoka. Jambo hilo wamesema ndilo linalochelewesha mabadiliko katika vyombo vya habari kwani wafanyikazi ni wale wale miaka nenda rudi.

Ni ukweli usiopingika kwamba kuanzishwa kwa vyombo vingi vya habari hakujaleta mabadiliko kama ilivyotarajiwa. Badala yake tumekuwa na wingi wa redio ambazo huwezi kuzitofautisha, kwani karibu zote zinatangaza mtindo mmoja.

Akitumia uzoevu wa miaka 24 katika kazi hiyo, Mmanga aliwaonya vijana wanaoibukia siku hizi kutangaza. Alisema inakera kuwasikia wakitumia muda mwingi katika kipindi kujijulisha majina yao."Kitaaluma ukishataja jina mwanzo wa kipindi, unalitaja tena mwishoni, na siyo kila baada ya dakika mbili." Aliongeza gwiji huyo aliyebobea katika fani ya utangazaji.

Kwa wakazi wengi wa Afrika mashariki na kati, sauti ya Ali Salim Mmanga siyo ngeni masikioni mwao. Kila Jumamosi saa nne asubuhi mpaka saa tano kasoro robo, hupeperusha hewani kipindi maarufu cha wajue wanamuziki. Utafiti uliofanywa na Injili unaonyesha kuwa kipindi hicho kina mashabiki wengi sana jambo ambalo limekipatia wadhamini wengi, na kuwaingizia KBC mamilioni ya shilingi kila kinaporushwa hewani. Hawawezi kukiri hadharani, lakini Mmanga ni kivutio kikubwa cha matangazo ya biashara ambayo ni uti wa mgongo wa KBC. Kwa sasa Mmanga ni mtayarishaji wa vipindi daraja la kwanza. Alizaliwa miaka 47 iliyopita katika kijiji cha Zibani Ngombeni, wilaya ya Kwale mkoa wa Pwani. Alisomea katika shule ya msingi Ngombena na baadaye kujiunga na elimu ya sekondari huko Alidina Visram katika mkoa wa pwani.Alipomaliza shule mwaka 1974 alianza kuifanyia kazi kampuni ya sigara akiwa kama muuzaji kwa mwaka mmoja kabla ya kujiunga na Securricoambapo pia alifanya mwaka mmoja mpaka mwaka 1976 alipojiunga na KBC, wakati huo ikijulikana kama VOK. Akijibu swali kama siku moja ataokoka, alisema: "Mimi ni mwisilamu mwenye msimamo." Ninasali mara tano kwa siku. "Sivuti sigara na wala sinywi pombe." Mimi siyo kama wengine ambao wana majina ya Yohana, Paulo na huku wanakunywa pombe."Ushauri wake kwa Wakristo: "msiwe wanafiki, bali yafuateni yote yaliyoandikwa katika msaafu wenu yaani Biblia." Na kwa watangazaji wenzangu, wawasikilize wale waliowatangulia ili wajifunze kutoka kwao."Siwezi kusema sijapata matatizo kazini, ila kila siku ninajitahidi kuyatatua. Alimaliza Mmanga ambaye ukiktana naye utafikiri ni kijana wa miaka 25. Ameoa huko Tanga Tanzania, na ana watoto wanne. Ukimuonna ni msafi wakati wote. huyo ni Mmnga.

<<back      Home   Gazeti La Injili    Injili3   Next>>