Injili na siasa
Dini na siasa siyo kwamba haziwezi kuchanganywa, bali moja iko kimakosa duniani. Siasa haiwezi bila dini, lakini dini inaweza pasipo siasa, kwa hiyo tunataka dunia isiyo na kitu kinachoitwa siasa.

Dini ni itikadi au imani inayomhusu mwanadamu na Mungu, wakati siasa ni itikadi au imani inayomhusu mwanadamu na mwanadamu. Siasa ni mwanadamu kumdanganya mwanadamu mwenzake kuwa anaweza kumsaidia mambo yote yanayomhusu hapa duniani bila Mungu, wakati dini inaweza kwa hakika kumsaidia mwanadamuhapa duniani na baadaye inamhakikishia uzima wa milele mbinguni.

Kwamba wanasiasa wanataka waachiwe siasa, na wahubiri wanataka kuingia siasa , hawa wote wawili wamechanganyikiwa. Ukweli ni kwamba lazima moja kati ya siasa na dini ikome kufanya shughuli zake kwa wanadamu.

Na kwa sababu dini inaweza kumsaidia mwanadamu kiroho na kimwili, basi lazima siasa isimamishe mara moja shughuli zake duniani kote. Yenyewe ndio inayojaribu kuyachukua majukumu ya Mungu kumwongoza na kumsaidia mwanadamu wakati inajua fika kuwa haiwezi.

Ukiwasikia wanasiasa wakiwaambia viongozi wa kidini waachane na siasa, waambieni kuwa wao ndio wanaotakiwa kuachana na siasa ili wajiunge na dini, maana dini ni mambo yote. Ya hapa duniani na ya huko mbinguni. Hakuna kiongozi wa kidini atakayethubutu kuiacha dini ajiunge na wanasiasa waongo na matapeli. Nawaita matapeli kwa sababu wanaitawala dunia kinyume na mwenye dunia alivyopanga itawaliwe. Mungu alipanga dunia itawaliwe na watumishi wake aliowaita na siyo wanasiasa waliojiweka madarakani kwa njia zisizo halali. Waulize viongozi duniani kote swali hili: Nani aliwatawaza kuwa viongozi? na utashangaa kusikia majibu yao.

Wengine watasema walichaguliwa na watu katika uchaguzi ulio kuwa huru na haki, kumbe rushwa ndio iliutawala uchaguzi. Afrika tuna viongozi waliochaguliwa katika mazingira ya ajabu sana.

Wananchi wanaaza kudanganywa na vyombo vya habari kwani karibu wote wanaosikika au kuonekana kwenye vyombo hivyo wakati wa uchaguzi mkuu lazima wawe walitoa rushwa.

Cha ajabu ni kwamba baada ya uchaguzi vyombo hivyo hivyo ndio vinakuwa mstari wa mbele kulaani rushwa ndani ya viongozi wale wale walioingia uongozini kirushwa. Ikiwa wao walipokea wakati ule, basi wana haki gani kuwakataza viongozi wasipokee ili kurudisha pesa zao. Jamii imetumbukizwa katika dimbwi la rushwa na wale ambao walitakiwa wawe wa kwanza kuipiga vita.

Ni mpaka utaratibu unaotumika kuwachagua viongozi ubadilishwe, ndipo tunapoweza kusema kuwa tuna jamii ambayo haina rushwa. Tumuache Mungu atuchagulie viongozi ambao wataongoza kwa kuzingatia yale Mungu anayoyataka. Pia wale viongozi walioko wakitubu na kuisikiliza sauti ya Mungu na kuitii, basi nchi zao zitakuwa na baraka tele.

Mungu anasema kuwa wanasiasa waachane na siasa na wajiunge na Injili ya kweli ya Yesu mwokozi. Watubu dhambi zao zote na Yesu atawasamehe na kuwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu.

Baada ya hayo wangoje kuisikia sauti yake Mungu ikiwaita katika uongozi.

<<back      Home   Gazeti La Injili    Injili3  Next>>