Dini zote ni sawa

Kila mwenye Dini huamini kuwa dini yake pekee ndio nzuri kuliko zile nyingine. Na angelifurahia kama dini zote zingelimalizika ibaki ya kwake tu ikitamba. Hayo ni mawazo potovu, na makala haya yatayarekebisha.

Ukweli ni kwamba dini zote ni sawa ila katiba ndizo zinazotofautiana. Na tofauti ya katiba haizifanyi ziwe tofauti kwani kwenye kila dini ni wachache wanaoifuata katiba ya dini yao na wengi hata hawaijui inasema nini.

Pengine mawazo ya kujiona bora kuliko wengine yanachangiwa na mbinu za kuwafanya watu wengi zaidi wajiunge kwenye dini hiyo, au kuwafanya wale waliokwisha jiunga tayari kutokuwa naawazo ya kuihama dini hiyo.

Kwa hiyo naweza kusema kwa ujasiri kuwa mbinu zinazotumika kuwafanya watu kuwa wamini, ndizo chanzo cha tofauti nyingi za kidini. Ambazo kama hazitaangaliwa kwa makini ni kama bomu linalongojea kulipuka.

Kwa sababu mimi ni Mkristo ebu nitoe maoni machache kuhusu Ukristo na jinsi ambavyo ungetakiwa upelekwe kwa wale ambao siyo Wakristo.

Imani ya Mungu kupitia kwa mwana wake Yesu Kristo ni imani inayohubiriwa kwa watu waliokubali kwa hiari yao wenyewe kusikiliza, bila kushurutishwa au kushawishiwa na kitu chochote mbali na upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Mhubiri mkuu wa imani hiyo Yesu Kristo hakutumia vishawishi vya mali au vitu vya dunia hii kuwafanya watu wawe Wakristo, wala hakuwalazimisha. Kinyume chake aliwatangazia yale aliyoyaamini kwa upendo, nawao kwa hiari yao wakaamua kumwamini au kuyakataa maneno yake.

Na leo hii mwamini yeyote ana haki ya kuyanena yale anayoyaamini kwa watu wote wenye dini na wasiyo nayo, na watu wana hiari yakumsikiliza au kutokufanya hivyo.Wale watakaomsikiliza, wana haki ya kufanya hivyo, na wale watakaokataa pia wana haki ya kufanya hivyo.

Tena wale walio yaamini maneno yake wana haki ya kujiunga na dini yake, na watakapofanya hivyo wasisumbuliwe na mtu yeyote kwani hatua walioichukua ni moja ya haki zao.Kwa sababu mtu ana haki ya kuiamini dini anayoitaka na pia ana uhuru wa kuhama dini hii kwenda ile nyingine.

Dini zote waumini wake ni watu, na watu siku zote wana matatizo yao. ni matatizo hayo ya watu ndio yanayozifanya dini zote kuwa sawa.Katika kila dini kuna wale waumini wa kweli, na wa bandia.Na siku zote wale wa bandia ndio wanaokuwa wengi. Kama huamini, nionyeshe dini isiyo na waumini bandia nami nitakuwa wa kwanza kuwaagiza watu wote wajiunge nayo.

Na kwa sababu hakuna ndio maana nawaagiza watu wote watubu dhambi zao wamwamini Yesu, ambaye atawapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu.Na ya kale yatapita tazama yatakuwa mapya.Na hawa waliofanyika Wana ndio ambao anawaandalia makao Mbinguni atakaporudi wakati wowote kutoka sasa, awachukue Mbinguni, bila kujali ni wa dini gani kwani wote wana dini moja ya Kuokolewa na Yesu. Na hao waliookoka siyo lazima wawe wa dini moja, maana dini zote ni sawa.

Imeandikwa na Munishi.

<<Back  |   Home |  Gazeti La Injili | Injili1 | Nyimbo Za Munishi | Next >>