Dini ya kweli kuiongoza dunia, siyo siasa

Siasa ni dini ambayo waumini wake wanawaamini viongozi wake ambao ni wanadamu. Mara nyingi siasa inadai inaweza kumsaidia mwanadamu hapa duniani, wakati ukweli wa mambo haiwezi. Mungu pekee ndiye anayeweza kumsaidia mwanadamu katika maeneo yote ya kiroho na kimwili.

Wanasiasa wamekuwa wakiwadanganya watu wa Mungu kuwa wao ndio jibu la kila tatizo. Huku wakitumia vitu alivyotuwekea Mungu tuvitumie kwa manufaa yetu. Wanachukua katika vilivyo haki yetu, na kutupimia ili tuwaamini wao badala ya mwenye vitu vyote ambaye ni Mungu.

Kwa sababu siasa yenyewe ni dini, imekuwa ikipinga dini zote za kweli kwani hizo ni tishio kwao. Ndio maana dini zote lazima zipate kibali kutoka kwao ili zimwabudu Mungu. Isitoshe wao ndio wanaopanga dini gani inayostahili kupewa au kutopewa kibali hicho. Mambo hayo hayastahili kuwa hivyo kwani Mungu alipomuumba mwanadamu alimuamuru amwabudu yeye peke yake. Wakati umefika wa dini zote kuamka kutoka kwenye usingizi wa miaka mingi, na kuanza kudai haki zao za kumwabudu Mungu bila kuwaogopa wanasiasa.

Ni makosa makubwa kwa mtu wa dini ya Mungu wa kweli kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa, kwani akifanya hivyo atakuwa anaamini katika dini mbili. Naye Mungu anatutaka tusimchanganye na chochote katika kumwabudu.

Ninachotaka kusema ni kwamba Dunia pamoja na vyote vilivyoko ni mali ya Mungu, naye ndiye anayetakiwa kuiongoza dunia na wala siyo siasa. Matumaini yangu ni kwamba vyama vya siasa vitaachia ngazi kwani dunia ya sasa itakuwa bila siasa.

Agizo langu kwa wote wenye dini ya Mungu wa kweli ni waache kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa, na waanze mikakati ya kuchukua madaraka ya kuiongoza dunia sawasawa na mapenzi ya Mungu. Vyama vya siasa vinalinda maslahi ya watu, na sisi tulinde maslahi ya Mungu ndani ya dunia ya Mungu.

<<back    Home   Gazeti La Injili    Injili3  Next>>